Wenger asema Arsenal ikivurunda ataondoka

Maneja Arsene Wenger amesisitiza "moyo wake upo kwa" Arsenal na ataondoka iwapo tu timu hiyo haitafanya vizuri.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Wenger aweka mambo sawa kwa Arsenal

Wenger, ambaye sasa ana umri wa miaka 62, aliliambia gazeti la L'Equipe kwamba ataangalia nafasi yake katika klabu hiyo msimu ujao.

Baada ya Arsenal kuilaza Norwich mabao 2-1, alikieleza kipindi cha michezo cha televisheni ya Sky: "Yalikuwa ni mazungumzo yaliyohusu iwapo sitafanya vizuri zaidi."

"Nilisema hiyo ndio njia pekee nitakayofikiria, iwapo nitakuwa chini klabu itakuwa huru kufirikia kitakachofuata."

Aliongeza: "Arsenal ni klabu ya maisha yangu na naheshimu mkataba wangu. Kwa upande wangu, nadhani kila mara nimekuwa nikijitoa kwa klabu yangu.

"Mwanzoni mwa msimu, watu wengi walikuwa wakiuliza ninafanya nini, lakini moyo wangu upo kwenye klabu ya Arsenal.

"Nawajibika kwa ukweli kabisa kupima kiwango cha ubora wa kazi yangu mwishoni mwa msimu na kujiuliza nimefanya kazi yangu kwa kiwango cha juu kwa timu?

"Unataka sasa niseme iwapo sitaipeleka Arsenal katika nafasi nne bora, kwa hiyo niondoke, ni jambo ambalo kamwe sitalisema."