Mancini aonesha wasiwasi Ubingwa Ulaya

Meneja wa Manchester City Roberto Mancini amesema timu yake ina nafasi asilima 30 tu kuweza kufuzu katika timu 16 kuwania Ubingwa wa vilabu vya Ulaya baada ya kulazwa na Napoli.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Roberto Mancini aonesha wasiwasi wa kusonga mbele

City walifungwa mabao 2-1 mechi iliyochezwa Italia siku ya Jumanne na sasa itahitaji kuifunga Bayern Munich halafu sala zao wazielekeze kwa Villarreal angalao watoke sare watakapocheza na Napoli, iwapo watahitaji kusonga mbele hatua inayofuata.

"Lengo letu ni kusonga mbele hatua ya pili na sasa tunategemea timu nyingine," alisema Mancini.

Mancini ameweka kipimo cha kusonga mbele asilimia 70 kwa Napoli na wao asilimia 30 tu.

Napoli walipigana kiume, lakini uzito wote wanauweka kwa Villarreal ambao wana wasiwasi watachezesha kikosi imara licha ya Wahispania hao kutokuwa na matumaini yoyote ya kusonga mbele.

"Iwapo Villarreal watacheza mchezo wao wa kawaida huenda wakapata matokeo mazuri," alisema. "Iwapo wataingia uwanjani kwa nia ya ushindi tuna matumaini ya kusonga mbele.

"Lakini wanapewa nafasi kubwa na haitakuwa mwisho wa maisha iwapo hatutafanikiwa kusonga mbele.

Ferguson aonesha matumaini

Naye meneja wa Manchester United Sir Alex Ferguson anaamini kikosi chake kitafuzu hatua ya mtoano ya Ubingwa wa Vilabu vya Ulaya licha ya kutoka sare na Benfica.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Sir Alex Ferguson aonesha matumaini ya kusonga mbele

United inahitaji angalao pointi moja watakapokabiliana na Basel katika mechi yao ya mwisho ya kundi C ili ifuzu hatua inayofuata baada ya matokeo ya Jumanne ya sare ya 2-2 na Benfica.

Lakini matumaini ya kuongoza katika kundi lao ni finyu kutokana na Benfica mechi yao ya mwisho watakabililiana na Otelul Galati isiyokuwa na pointi hata moja na imeonekana dhaifu katika kundi lao.

"Utakuwa mchezo mgumu dhidi ya Basel. Lakini nina imani na kikosi changu," alisema Ferguson.

"Benfica lazima watashinda dhidi ya Galati lakini tunahitaji kushinda kwa mbwembwe."

Wakimaliza nafasi ya pili katika kundi lao itakuwa na maana Manchester United huenda mapema wakakabiliana na timu kama Barcelona, Real Madrid, Inter Milan au Bayern Munich katika hatua ya timu 16 za mwisho, lakini Ferguson hana wasiwasi na hilo.