Mancini akataa kujadili Tevez

Meneja wa klabu ya Manchester City Roberto Mancini amekataa kuzungumzia majaliwa ya mchezaji wa klabu hio Carlos Tevez wakati wa vikao vyake vya kila wiki akitazamia mchuano wa jumapili dhidi ya Liverpool.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Kocha akataa kujadili Tevez

Inafahamika kuwa Mshauri wa Tevez, Kia Joorabchian alikutana na wakuu wa klabu ya AC Milan nchini Italia kwa matumaini kuwa anaweza kufikia makubaliano ya kusajiliwa na klabu hio. Kwa wakati huu Tevez hashiriki hata mazowezi na wenzake katika klabu ya Manchester City kwa sababu ambazo hazijaelezwa.

Endapo City itapokea ombi linalostahili kiwango cha mchezaji huyo anaweza akaruhusiwa kuondoka na siyo kwa mkopo wa mda.

Hata hivyo, Mancini hakutaka kujadili lolote kumhusu mchezaji aliyeasi mamlaka yake.

Amewambia wandishi habari kuwa sitaki kuzungumza kuhusu Carlos Tevez.

Mancini alipenda kuzungumzia kipigo klabu yake ilichokabili huko Itali kwenye mchuano dhidi ya Napoli 2-1.

City inahitaji kuifunga Bayern Munich katika mechi ya mwisho kuhakikisha kuwa inapiga hatua katika mashindano ya Ligi ya mabingwa barani Ulaya.

Mancini ana imani kuwa hilo linawezekana,ingawa watategemea matokeo baina ya Villareal na Napoli pia.

Hata hivyo, Mancini amesema kuwa hadhani kama City inaweza kushinda Kombe la Ligi ya mabingwa msimu huu.

Kwa mtazamo wake ameonelea kuwa vilabu kama Real Madrid, Bayern Munich na Barcelona ndiyo vyenye uzowefu kwenye mashindano haya kuliko City.