Villas Boas akataa msaada

Ligi kuu ya England inatazamia mechi kali wikendi hii na macho yote yanamtazama kocha wa klabu ya Chelsea Andre Villas-Boas.

Kocha huyo amesema hahitaji msaada kutoka kwa mtu yeyote kufuatia mapendekezo kuwa huenda atahitaji msaada wa kocha mwingine mwenye uzowefu kuingo'a klabu yake kutokana na mdororo inaopitia.

Chelsea inachuana na Wolverhampton Wanderers jumamosi kuanzia saa kumi na mbili za Afrika ya mashariki. Kocha huyo alipoulizwa kama angefurahia msaada wa kocha mkongwe Guus Hiddink, Villas Boas alikataa kujibu ingawa alikiri kuwa kulikuepo na mkutano wa dharura siku ya jumatano kufuatia mechi ya Ligi ya mabingwa ambapo ilichapwa na Bayer Leverkusen 2-1. Kocha huyo amesema kuwa mabadiliko ni muhimu, lakini hatobadili mbinu zake wala nyenzo za utendaji kazi. Baada ya kupoteza mechi nne mfululizo kati ya mechi saba za Ligi katika kile kinachotajwa kama mwanzo mbovu tangu enzi ya Roman Abramovic ianze mnamo mwaka 2003.

Kwa mechi dhidi ya Wolves Villas Boas anataraji kumrejesha Ashley Cole aliyepona jeraha.

Wolves, ambayo inashikilia nafasi ya 17 ikinusia shoka la kudidimizwa nje ya Ligi kuu ya England, itawakosa wacheza kiungo wawili Jaime O'Hara and Stephen Hunt wakitafuta ushindi kwenye uwanja wa Stamford Bridge kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1979. Manchester United ambayo pia itaingia uwanjani wakati mmoja mechi ya Chelsea na Wolves ikichezwa itakosa huduma za mcheza kiungo M'Brazili Anderson ambaye inasemekana hatogusa gozi hadi mwezi Febuari kutokana na maumivu ya goti.

Manchester United inachuana na Newcastle United kwenye uwanja wa Old Trafford.

Habari nzuri kwa Sir Alex Ferguson ni kwamba mshambuliaji wake mahiri, Wayne Rooney amepona maumivu ya nyonga. Klabu hiyo inamkosa pia Tom Cleverly ambaye pia ni majeruhi.

Klabu ya Stoke itakosa huduma za msghhambuliaji wake Peter Crouch ambaye pia ana maumivu ya nyonga wakati klabu yake ikichuana na Blackburn iliyo katika nafasi ya 19.

Blackburn haitazamiwi kuwa na wachezaji wake kadhaa ikiwa ni pamoja na beki Chris Samba na Martin Olsson,pia Ryan Nelson huku mcheza kiungo David Dunn anatumikia kifungo cha kadi nyekundu.

Baada ya kupoteza mechi tisa mfululizo kati ya 12 za ufunguzi, Bolton Wanderers iliyo katika nafasi ya 18 kwenye msimamo wa Ligi itahitaji udhibiti ulinzi wake ili kupata ushindi wa tatu kwenye uwanja wake itakapoipokea Everton iliyo katikati mwa orodha Ligi.

Klabu ya Sunderland inayozidi kudidimia itachuana na Wigan Athletic kwa mpambano wa walala hoi. Hadi wakati huu Wigan imeweza kufunga jumla ya mabao 10 pekee huku Sunderland ikiwa na jumla ya mabao 14. Klabu ya jiji la London inayotamba Tottenham Hotspur, iliyojikuta katika nafasi ya tatu inaweza kupata ushindi wake wa kwanza dhidi ya West Bromwich Albion tangu mwaka 2003.

Ratiba ya jumamosi ina mechi 8 ambapo goalkipa wa Arsenal Wojciech Szczesny amewaonya wachezaji wenzake wasiipuuze Fulham licha ya Arsenal kushinda mechi 11 kati ya 13 na kufanikiwa kufuzu kushiriki michuano ya 16 za mwisho katika Ligi ya mabingwa barani Ulaya.

Fulham ni mojapo ya Timu ngumu katika Ligi ya England na Szczesny ambaye aliongezea kusema kwa hadhani kama watakua na shida kucheza bila mchezaji Carl Jenkinson na Kieran Gibbs.

Fulham, imo katika nafasi ya 16 haijawahi kushinda ugenini kwenye uwanja wa arsenal. Manchester City iliyo kieleleni mwa Ligi ya England inachuana na Liverpool jumapili.