Wakenya wawika Kampala

Wakenya waliendelea kuonyesha umahiri wao katika mashindano ya riadha na ya tisa ya MTN marathon mjini Kampala.

Mkenya James Kariuki Mbugua aliibuka mshindi katika mashindano hayo ya kilomita 42, na kupata zawadi ya shilingi milioni 16 za Uganda, sawa na dola za Marekani 6,000.

Image caption Aliwaongoza Wakenya katika kung'ara katika mbio za marathon Kampala

Alimaliza kwa muda wa saa 2:16:46.

Wakenya wenzake, James Yatich na Ernest Kipruto, walimaliza katika nafasi ya pili na tatu, na kupata dola 3,000 na dola 1,500.

Zaidi ya wanariadha 20,000 walijitokeza katika uwanja mdogo wa ndege wa Kololo, kushiriki katika mashindano hayo ya mwaka 2011 yaliyofanyika siku ya Jumapili.

Wengi ya wanariadha hao walitoka katika mataifa ya Kenya, Tanzania, Rwanda, Ethiopia, Eritrea na wenyeji Uganda.

Kwa upande wa mashindano ya kina dada, Jane Suuto kutoka Uganda alimaliza katika nafasi ya kwanza, kwa muda wa saa 2:47:44.

Image caption Dorcus Inzikuru akibebewa juujuu baada ya kushinda nusu-marathon

Dinknesh Tefera kutoka Ethiopia alikuwa wa pili, na Rose Kiboino kutoka Kenya akamaliza katika nafasi ya tatu.

Senti zilizokusanywa kupitia mashindano hayo zitaelekezwa katika wilaya ya Amuria, kusaidia katika kuwasaidia wakaazi kupata maji safi.

Hukohuko Uganda, raia wa nchi hiyo, Flavia Namakula, amehifadhi tena taji la golf ya wanawake katika mashindano ya Uganda Open, mashindano yaliyomalizika uwanja wa Kintante mjini Kampala. Mashindano ya mwaka huu yalishirikisha wachezaji kutoka Tanzania, Zimbabwe na wenyeji Uganda.