Arsenal na Chelsea zatolewa Carling Cup

Bao la dakika za mwisho lililofungwa na Sergio Aguero liliipatia Manchester City ushindi wake wa kwanza nyumbani kwa Arsenal kwa kipindi cha miaka 36 na kujipatia nafasi ya kucheza nusu fainali ya Kombe la Carling.

Haki miliki ya picha PA
Image caption Sergio Aguero akishangilia bao

Park Chu-young na Alex Oxlade-Chamberlain wakati wa kipindi cha kwanza walijaribu mikwaju ambayo haikuzaa matunda katika lango la Manchester City.

Lakini Edin Dzeko mshambuliaji wa Manchester City mara tatu mikwaju yake haikulenga lango, ingawa katika dakika ya 83 ndiye alikuwa chachu ya ushindi.

Baada ya kona waliyopata Arsenal na kushindwa kufunga, mpira ukawa unaelekea upande wa Arsenal na pasi ya Dzeko ilinaswa na Adam Johnson aliyemsogezea Aguero ambaye alipachika bao lake la 12 kwa msimu huu.

Ilikuwa ni pigo kwa Arsenal ambao kwa muda mrefu wa mchezo walikuwa wakionekana wangeweza kushinda pambano hilo.

Meneja wa Arsenal Arsene Wenger alisema baada ya mchezo: "Hayakuwa matokeo ya kupendeza, lakini kwa kipindi fulani tulionekana tumezubaa. Nahisi hatukutumia vizuri kona tulizozipata lakini kwa ujumla kinachokera tumepoteza mchezo ambao tulionekana tungeshinda.

Chelsea kwa mara nyingine iligonga kisiki cha Kenny Dalglish wakati Liverpool iliendelea kuzidisha mapigo ya moyo kwa meneja wa Chelsea Andre Villas-Boas baada ya kushinda mabao 2-0 katika pambano jingine la robo fainali ya Kombe la Carling Cup katika uwanja wa Stamford Bridge.

Maxi Rodriguez na Martin Kelly walipachika mabao hayo mawili kwa kupishana dakika tano na kuendeleza rekodi ya Dalglish ya kutofungwa na Chelsea katika michezo 13 tangu alipochukua hatamu za kuwa meneja wa Liverpool.

Ushindi wa Liverpool ulionekana dhahiri, licha ya kumpumzisha mpachika mabao wao hatari Luis Suarez na waliweza kuibuka vizuri hata baada ya Andy Carroll kukosa kufunga mkwaju wa penalti, wakiendeleza ushindi wao tatu mfululizo katika uwanja wa Stamford Bridge.