O'Neill akubali kuiongoza Sunderland

Martin O'Neill amekubali kuwa meneja wa Sunderland, baada ya Steve Bruce kufutwa kazi.

Lakini O'Neill, ambaye kibarua cha mwisho kama meneja ilikuwa ni katika klabu ya Aston Villa, hataweza kuiongoza timu hiyo katika mechi ya Jumapili ya ugenini dhidi ya Wolverhampton.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Meneja mpya wa Sunderland

Sunderland imethibitisha kwamba aliyekuwa msaidizi wa Bruce, Eric Black, atakuwepo uwanjani kusimamia mechi hiyo.

"Paka weusi", kama wanavyojulikana Sunderland, wameahidi kutoa taarifa hivi karibuni kuhusiana na meneja wao mpya.

O'Neill alikuwa ametajwa mara kwa mara kama mtu ambaye angeliweza kuchaguliwa kuviongoza vilabu mbalimbali katika kipindi cha miezi 12 iliyopita, na wengi walitazamia ataipata kazi hiyo ya Sunderland.

Sunderland hivi sasa imo katika nafasi ya 16, ikiwa imevuka hatari ya kushukishwa daraja kwa pointi mbili tu, na ndio sababu hasa iliyosababisha Bruce kufutwa kazi Jumatano iliyopita.

Kati ya mechi zao 13 msimu huu, Sunderland imepata ushindi katika mechi mbili tu.

O'Neill, mwenye umri wa miaka 59, aliwahi kuichezea Nottingham Forest, lakini sifa zake kama meneja ni wakati alipoiongoza Wycombe Wanderers, kabla ya kuviongoza pia vilabu vya Leicester City na Celtic.

Aliingia Villa mwaka 2006 na kuiwezesha kumaliza katika nafasi ya sita katika ligi kuu ya Premier, misimu mitatu mfululizo, na vile vile kuifikisha katika fainali ya Kombe la Carling, kabla ya kujiuzulu kabla ya kuanza kwa msimu wa mwaka 2010-11.

Inafahamika kwamba tayari amekutana na tajiri ambaye anamiliki Sunderland, na ambaye pia ni mwenyekiti wa timu, Ellis Short, Alhamisi jioni, na hasa kuelezewa juu ya hali ngumu kwa upande wa bajeti katika uwanja wa Stadium of Light.