MYSA yapata tuzo

Methembe Ndlova na Peter Karanja
Image caption Nahodha wa Zimbabwe Warriors akimkabidhi Peter Karanja tuzo ya uongozi bora katika michezo

Mathare Youth Sports Association, (kwa kifupi MYSA), ambacho ni chama cha vijana wanaojizatiti katika kutumia michezo kupata maendeleo katika jamii, siku ya Ijumaa, tarehe 9 Desemba, kimepata tuzo katika mkutano wa dunia wa michezo mjini Cape Town, Afrika Kusini.

Tuzo hiyo ya uongozi bora katika michezo, inatambua juhudi za MYSA za kuanzisha mipango mbalimbali kimichezo, na ambayo imeweza kufanikisha kupata maendeleo ya kijamii nchini Kenya katika kipindi cha miaka 25 iliyopita.

Afisa mkurugenzi mkuu wa MYSA, Peter Karanja, alipokea tuzo hiyo kwa niaba ya viongozi na vijana 25,000 wa MYSA.

Wengine ambao wameshawahi kupokea tuzo hiyo ya Beyond Sport Judge's Award ni pamoja na aliyekuwa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan (2009), na familia ya Shriver ya nchini Marekani (2010), na ambao ni waanzilishi wa mashindano ya Olimpiki kwa walemavu.

MYSA walikuwa wabunifu kwa kutumia michezo katika kuimarisha maisha bora katika jamii, hasa kwa kuanzisha mipango kama ile ya kuzoa takataka katika mitaa ya mabanda, kuimarisha mazingira bora, na vile vile kuendesha kampeni za kuzuia kuenea kwa viini vya HIV na ugonjwa wa ukimwi.

Miaka 25 tangu MYSA kuanzishwa, hili ndio kundi kubwa zaidi barani Afrika la vijana wanaojitegemea hasa kwa kutumia michezo na kufikia viwango mbalimbali vya ufanisi katika maendeleo ya jamii.

Moja kwa moja, vijana 200,000 wamenufaika kupitia mipango ya MYSA.

Umri wa kadri wa vijana hao, kuanzia wanachama hadi makocha na viongozi wao, ni kati ya umri wa miaka 15-16.

Zaidi ya wahusika 400, kulingana na Beyond Sport, na kutoka mataifa 125, walikuwa wakiwania tuzo hiyo.