Wenger apongeza ukakamavu wa Arsenal

Meneja wa Arsenal Arsene Wenger amewasifu wachezaji wake baada ya kuzinduka kutoka usingi wa mwanzo mbaya msimu huu wa ligi, baada ya kuilaza Everton na kusogea hadi nafasi ya nne.

Haki miliki ya picha a
Image caption Arsene Wenger awasifu wachezaji wake

Arsenal walipoteza michezo minne kati ya michezo saba ya ufunguzi wa Ligi Kuu ya Kandanda ya England lakini sasa mambo yao yamekaa vizuri wakiendelea kujizolea pointi.

"Tulikuwa na mwanzo mbaya sana lakini sasa tumeimarika," Wenger alisema hayo baada ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Everton.

"Ari yetu ni nzuri, tuna malengo. Tunahitajika kuimarika kwa kiwango cha juu. Iwapo tutaendelea kuidhibiti hali hiyo basi tutakuwa na nafasi nzuri."

Ushindi wa Arsenal umewapandisha hadi nafasi ya nne juu ya Chelsea watakaopambana na vinara wa ligi hiyo hadi sasa, Manchester City siku ya Jumatatu.

Wameendeleza wimbi la ushindi tangu walipopoteza kwa mabao 2-1 dhidi ya Tottenham tarehe 2 mwezi wa Oktoba wakati huo walipokuwa nafasi ya 15 na pointi saba.

Wenger alisema:"Katika baadhi ya mikutano na waandishi wa habari nimekuwa nikisema hatuchezi kwa ajili ya kuepuka kushuka daraja kwa hiyo usingeweza kutabiri kama tutakuwa katika nafasi tuliyonayo."

"Tupo katika nne bora na iwapo Chelsea watashinda siku ya Jumatatu watakuwa juu yetu."

Habari zaidi za ligi kuu ya Premier ni kwamba viwanjani, katika mechi za Jumapili, Stoke iliwazaba Tottenham magoli 2-1.

Mechi ya awli kati ya Sunderland na Blackburn nayo ilimalizika kwa idadi hiyo ya magoli, wakati Sunderland walipoibuka washindi 2-1.