Kulazawa Tottenham alaumiwa mwamuzi

Meneja wa Tottenham Harry Redknapp amekasirishwa na mwamuzi Chris Foy baada ya kufanya uamuzi ambao ulikuwa na mashaka wakati timu yake ilipofungwa mabao 2-1 na Stoke.

Image caption Harry Redknapp amlaumu mwamuzi Chris Foy

Spurs inahisi Foy hakuona mara mbili wachezaji Stoke walipounawa mpira, na kulikataa bao la Emmanuel Adebayor kwa madai ya kuotea na kwa kumtoa nje kwa kadi nyekundu Younes Kaboul.

"Adebayor hakuotea," alisema Redknapp. "Kulikuwa na matukio mawili ya wachezaji kuunawa mpira na mwamuzi hakuona.

"Nahisi hakuwa na siku nzuri. Kumtoa nje kwa kadi nyekundu Kaboul ilikuwa ni makosa."

Stoke walipata mabao yao mawili kipindi cha kwanza yaliyopachikwa na Matthew Etherington, ingawa mpira ulionekana kumgonga mkononi Peter Crouch akijiandaa kumpasia Ethirington wakati wa kufungwa bao la kwanza.

Tottenham walijibu mashambulio kwa bao la mkwaju wa penalti lililopachikwa na Adebayor lakini walinyimwa nafasi nyingine za mikwaju ya penalti mara mbili wakati wakijitahidi kusawazisha.

Mpira aliopiga Kaboul langoni ulielekea kumgonga Ryan Shawcross katika kiwiko cha mkono na katika piga nikupige iliyofuatia baadae, bao la Adebayor lilikataliwa baada ya kuonekana ameotea.

Jermain Defoe pia mkwaju wake mmoja ulizuiwa kwa mkono na Tottenham baadae ikazamishwa zaidi baada ya Kaboul kutolewa nje kwa kadi nyekundu.

"Ndio maana tukaambulia patupu," alisema Redknapp. "Hatukucheza vizuri kipindi cha kwanza. Lakini tulibadilika kipindi cha pili na tuliwabana vilivyo.

"Kwa bahati mbaya baadhi ya uamuzi alioufanya mwamuzi ulikuwa na makosa makubwa."