Hearts wapokea mshahara

Hearts Haki miliki ya picha bbc
Image caption Wachezaji wa Hearts na zawadi kwa watoto katika hospitali ya Royal

Klabu ya Hearts imeweza kutoa malipo yote ya mshahara wa Novemba kwa wachezaji, huku chama cha wachezaji wa Uskochi, PFA, kikijiandaa kuwasilisha malalamiko rasmi kwa wahusika wa ligi kuu ya Premier ya nchi hiyo.

Wachezaji waliokuwa wamekerwa mno na hali ya mambo walikuwa wametoa huru kwa chama chao cha PFA kuchukua hatua kali kwa niaba yao, ikiwa wangelikosa malipo yao kufikia Ijumaa tarehe 16 Desemba 2011, wakati ambao wanatazamia mishahara ya mwezi huu.

Chama cha PFA kipo tayari kuchukua hatua ikiwa mishahara ya Desemba itacheleweshwa.

Mishahara ya Oktoba ilicheleweshwa kwa siku 16, na ile ya Novemba kwa siku 29.

Mkurugenzi wa klabu ya Hearts Sergejus Fedetovas katika tovuti ya timu ameandika: "Zogo hili lote kuhusiana na Hearts ni biashara mwafaka kwa vyombo vya habari, na hata miongoni mwa baadhi ya mawakili".

"Ninaweza kuwahakikishia mashabiki wa klabu kwamba juhudi za kuendelea na shughuli kama kawaida katika klabu, na pia tunafahamu sheria na utaratibu wa mambo - kwa hiyo hakuna wachezaji watakaoihama timu", aliongezea.