Cheruiyot ashamiri mwaka huu

Mwanariadha wa Kenya Vivian Cheruiyot anatarajiwa kua kwenye kilele cha wengi miongoni mwa wale wenye jukumu la kumchagua mwanariadha bora mwanamke wa mwaka huu wakuu wa shirikisho la riadha duniani- IAAF watakapokutana jumamosi.

Haki miliki ya picha Getty images
Image caption Vivian ashamiri mwaka 2011

Cheruiyot alishinda moja kati ya medali zake tatu za dhahabu kwenye mashindano ya Dunia ya mbio za nyika nchini Uhispania mnamo mwezi Machi. Mnamo mwezi wa Julai aliweka rekodi ya Jumuia ya madola katika mbio za mita 5,000 kabla ya kushiriki mbio za mita 5,000 na 10,000 kwa mpigo wakati wa mashindano ya Dunia mjini Daegu na baada ya hapo akaongoza mbio za Diamond mjini Zurich.

Hata wakati akikimbia hakuonesha dalili za uwezo wa kushinda, lakini alionyesha nguvu za ziada na uwezo wa kuwazidia wapinzani wake.

Kwenye mashindano ya mbio za nyika ya Dunia, hatua zake za mwisho kwenye mkondo wa kilomita 2 alimaliza kwa dakika 6 na sekunde 3 mda ambao ulikua wa kasi zaidi ya wanariadha wengi wanaume wa Uingereza siku hiyo.

Cheruiyot ameonyesha umakini licha ya kuongezea mbio za mita 10,000 hajaonyesha kuchoshwa na amezidi kushamiri katika mbio zake za kawaida ukizingatia ushahidi wa mda aliyouweka mjini Daegu wa 56.68 mzunguko wa mwisho katika mbio za mita 5,000. Mda huo ni sawa na ule wa sekunde 52 wa kasi aliyoitumia Mo Farah wa Uingereza, akifuatiwa na Bernard Lagat na wanariadha wa Ethiopia wanaume.

Zawadi ya Cheruiyot ni kwamba amechaguliwa na chama cha riadha cha Kenya kuiwakilisha nchi yake kwenye mashindano makubwa ya Olimpiki mjini London mwakani kwa kushiriki mbio za mita 5,000 na 10,000.

Ushindi wa medali tatu za dhahabu ni mafanikio ya mwanamke huyu Mkenya katika mbio za masafa marefu ambaye anastahili sifa na zawadi nono ya IAAF.