Mashabiki Botswana kutoshuhudia timu yao

Mashabiki wa kandanda nchini Botswana wamenyimwa nafasi ya kuishuhudia timu yao taifa ikishiriki mashindano yajayo ya Kombe la Mataifa ya Afrika.

Image caption Mashabiki wa kandanda Botswana kukosa uhondo wa mechi

Hatua hiyo imekuja baada ya serikali ya Botswana kugoma kununua haki ya kutangaza kutoka kampuni ya Ufaransa ya SportFive.

Serikali imesema gharama ya Pula milioni 15 sawa na dola za Marekani milioni 1.98 haziingii akilini.

Msemaji wa serikali ya Botswana Dokta Jeff Ramsaya ameiambia BBC kwamba kiwango cha Pula milioni 15 kuweza kupata haki ya kuangalia timu yao ya taifa ikishiriki katika mashindano hayo kimeonekana ni kikubwa sana.

Hatua hiyo imekuja baada ya majadiliano kuvunjika kati ya SportFive na Televisheni ya taifa (Btv), ambayo inaitegemea serikali kwa fedha.

"Kwa sasa tunakabiliwa na matatizo ya fedha katika bajeti yetu, kwa kweli tulitenga kiasi cha fedha katika bajeti na kiwango hiki hatukukiweka," Ramsay alieleza.

Aliongeza kueleza ana matumaini mashabiki wengi wa kandanda wataweza kufuatilia michuano hiyo kupitia televisheni za kulipia zinazoonesha mashindano hayo kwa kutumia mitambo ya setelaiti.

Ramsay ameongeza kusema serikali tayari imewekeza kiasi cha fedha kwa kuiandaa timu yao ya taifa inayoshiriki kwa mara ya kwanza mashindano hayo.

Serikali ya Botswana inagharamia mazoezi ya siku kumi ya timu hiyo iliyopiga kambi nchini Afrika Kusini katika kituo cha michezo cha Royal Bafokeng Sports mjini Rustenburg.

Baada ya kumaliza kambi huko Rustenburg, timu ya taifa ya Botswana maarufu Zebras ama Pundamilia itaelekea nchini Qatar tarehe 26 mwezi huu, ambapo watafanya mazoezi katika chuo cha Aspire Academy kwa gahrama za serikali.

Botswana wapo katika kundi D pamoja na Ghana, Mali na Guinea.

Wakati wa michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika nchini Angola mwaka 2010, Btv iliamriwa kusimamisha kutangaza fainali hizo baada ya kushindwa kukosa haki ya kuonesha -huku kampuni ya SportFive ikielezea kwamba Btv walionesha mechi ya ufunguzi kinyume na sheria.