Ahadi ya O'Neil kwa Ulimwengu wa Soka

Martin O'Neil na Peter Musembi
Image caption Sunderland ina nia ya kukifanya klabu maarufu kimataifa

Meneja mpya wa Sunderland Martin O’Neill anasema mchuano kati yao na Manchester City tarehe mosi Januari utakuwa mtanange wa hakika, na hiyo ni ahadi yake kwa wasikilizaji wa matangazo ya Ulimwengu wa Soka kupitia Idhaa ya Kiswahili ya BBC London.

Idhaa ya Kiswahili ya BBC itakuwa inatangaza mechi hiyo moja kwa moja kutoka uwanja wa Stadium of Light, mjini Sunderland.

Martin O’Neill anafahamu jinsi ligi ya primia ya Uingereza inavyofuatwa sana na mashabiki wengi Afrika mashariki na kati, na pia anafahamu siku hiyo watangazi wa Idhaa ya Kiswahili ya BBC watakuwa uwanjani kutangaza mchuano wao dhidi ya Man City.

“Naona fahari sana kwamba tunafuatiliwa kutoka maeneo mengi, barani Asia hadi Afrika mashariki. Hili linanipa furaha kubwa, kwa sababu najua Sunderland ni klabu kubwa tangu zamani, ni vile tu vilabu vingine ambavyo vina fedha nyingi vimeipiku,” O’Neill aliambia BBC Ulimwengu wa Soka.

Image caption Peter akiwa katika chumba cha kubadilishia mavazi cha Sunderland

‘’Lengo letu ni kuirejesha hadhi ya zamani ya Sunderland, na hiyo inawezekana.” Aliongeza.

Mechi hiyo inatarajiwa kuwa ngumu huku Man City wakipania kukaa kileleni kwenye msimamo wa Ligi, nao Sunderland wakidhamiria kupata matokeo mazuri ili kuimarisha nafasi yao.

Bwana O’Neill amewaahidi mashabiki Afrika mashariki kutazamia mchuano mkali.

“Nina hakika kutakuwa na fataki,” alisema.

Kuhusu mshambuliaji wa Ghana Asamoah Gyan ambaye aliondoka klabu hiyo kwenda kucheza Uarabuni kwa mkopo, Bwana O'Neil aliiambia BBC angetaka kumrudisha mchezaji huyo katika klabu baada ya kipindi cha mkopo, lakini akasema hatua kama hiyo itategemea Gyan mwenyewe, klabu anayoichezea na pia bodi inayosimamia Sunderland.

Wachezaji kutoka Afrika waliosalia katika Sunderland ni Stephane Sessegnon kutoka Benin, na Ahmed Almohamady kutoka Misri.

Benin na Misri hazikufuzu kushiriki fainali za kombe la mataifa ya Afrika, na hii inampa furaha Martin O'Neill kwamba wachezaji wake hawataondoka mwezi Januari kwenda kuwakilisha mataifa yao katika fainali hizo zinazoandaliwa kwa pamoja na Gabon na Equatorial Guinea.

“Ni furaha kwa sababu sitahitaji kupoteza wachezaji hawa muhimu kwa kipindi cha mwezi mmoja, na tutakapokuwa na mechi ngumu hiyo haitakuwa sababu yoyoye ya kuwa na wasi wasi.”