Yaya na Kolo wawekewa ngumu

Yaya Haki miliki ya picha AFP
Image caption Toure huenda akakosa mechi dhidi ya United

Kocha wa Ivory Coast Francois Zahoui amekataa ombi la Manchester City la kutaka Yaya Toure na Kolo Toure kucheza mechi ya Jumapili dhidi ya Manchester United ya kombe la FA.

"Vilabu vinafahamu kanuni," Zahoui ameiambia BBC. "Natarajia wawili hao kufika katika tarehe iliyopangwa na Fifa."

Meneja wa City Roberto Mancini aliomba Yaya na Kolo kucheza mechi ya Jumapili kabla ya kujiunga na kambi ya Ivory Coast.

Kwa mujibu wa sheria za Fifa, wachezaji wanatakiwa kuripoti kambini wiki mbili kabla ya michuano kuanza. Michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika inaanza Januari 21.

Haki miliki ya picha PA
Image caption Kolo Toure naye atakiwa kuripoti kambini

City na United ambao kwa sasa wanaongoza ligi ya England, watakutana kwenye uwanja wa Etihad katika raundi ya tatu ya kombe la FA siku ya Jumapili.

Katika mkutano na waandishi wa habari siku ya Alhamis asubuhi, Mancini alisema aliomba wachezaji hao wachelewe kuondoka.

Lakini Zahoui amesisitiza kuwa wachezaji hao waripoti mjini Paris Ufaransa kwa ajili ya mkutano siku ya Jumamosi kabla ya kusafiri na kikosi kizima cha Ivory Coast kwenda Abu Dhabi kwa ajili ya kambi ya mazoezi ya wiki mbili inayoanza Jumapili.