Kiprop ashinda mbio za nyika Scotland

Kiprop
Image caption Asbel Kiprop hatimaye ashinda Scotland

Bingwa wa dunia na Olimpiki Asbel Kiprop kutoka Kenya ameshinda kirahisi mbio za kilomita tatu kwa wanaume katika mbio za nyika za Great Edinburgh.

Alimaliza kwa dakika 9 na sekunde 20 na kumshinda Mwingereza Jonny Hay (9.25), huku Kenenisa Bekele wa Ethiopia akimaliza katika nafasi za chini.

Bingwa wa Ireland wa mbio za nyika Fionnuala Britton alishinda mbio wa wanawake za kilomita 6 kwa sekunde 21.32 mbele ya Gemma Steel na Elle Baker wa Uingereza.

"Ni vizuri kujisikia na nguvu na kukimbia vile," Britton ameiambia BBC Sport.

Kiprop alimshinda Mkenya mwenzake Brimin Kipruto, aliyeshinda dhahabu katika mbio za kuruka viunzi mita 3,000, na mkongwe kutoka Ethiopia Bekele, ambao wote walimaliza katika nafasi za chini. Bekele ambaye alishinda dhahabu katika mita 5,000 na 10,000 mjini Beijing mwaka 2008, anaonekana kama hasimu mkubwa kwa Mo Farah katika michuano ya Olimpiki ya London 2012, lakini alitatizwa na kasi.

Kiprop, 22, alisema: "Nilitarajia ushindani mkali"

"Nimefurahi kushinda hapa leo baada ya kushika nafasi ya pili mwaka jana."