Wenger amjia juu mwamuzi mechi ya Fulham

Meneja wa Arsenal, Arsene Wenger amesema mwamuzi Lee Probert ameigharimu timu yake kupoteza mchezo kwa kufungwa mabao 2-1 na Fulham.

Haki miliki ya picha getty
Image caption Wenger adai mwamuzi aliinyonga Arsenal dhidi ya Fulham

Arsenal walionekana dhahiri wangeondoka na pointi tatu katika uwanja wa Craven Cottage hadi pale wenyeji walipocharuka na kufunga mabao hayo mawili zikiwa zimesalia dakika tano kabla ya mpira kumalizika.

Wenger hakufurahishwa na uamuzi wa kumtoa nje kwa kadi nyekundu mlinzi Johan Djourou baada ya kuoneshwa kadi ya pili ya njano na pale waliponyimwa mkwaju wa penalti.

"Mwamuzi amesababisha matokeo yawe yalivyokuwa kutokana na kutoa uamuzi mbovu, hii kwa maoni yangu," alisema Wenger.

Arsenal sasa wanashikilia nafasi ya tano ya msimamo wa Ligi Kuu ya soka ya England, pointi moja nyuma ya Chelsea, kufuatia kupoteza mchezo wake wa tano ugenini.

Djourou alitolewa nje kwa kadi nyekundu katika dakika ya 78 kwa kosa la kumvuta na kumuangusha Bobby Zamora lakini Wenger anahisi mlinzi wake huyo alipewa adhabu kali na akaishutumu Fulham kwa kufanya mbinu kuhakikisha mlinzi huyo anatolewa nje.

"Wakati Djourou alipooneshwa kadi ya kwanza ya njano, walikuwa wanajaribu kufanya kila hila aoneshwe nyingine atolewe nje na mwamuzi aliingizwa mtegoni," alisema Wenger.

"Nilikuwa naiona kadi inakuja. Nisingependa kuwa chanzo cha habari cha magazeti. Nakuambia kile nilichokiona mchezoni. Sijali kitakachotoke."

Wenger pia anahisi timu yake ilipaswa kupewa penalti katika kipindi cha kwanza.

Alipoulizwa iwapo Gervinho alifanyiwa rafu ndani ya sanduku la hatari na Philippe Senderos, Wenger alisema: "Ni aslimia 200, lakini tulijua hatungepewa nafasi ya kupiga mkwaju wa penalti."

Arsenal ilitawala mchezo katika kipindi cha kwanza kwa bao lililofungwa kwa kichwa na Laurent Koscielny.

Fulham baadae ilijipatia ushindi kwa mabao yaliyofungwa na Steve Sidwell na Zamora katika dakika tano za mwisho.