Ferguson asema Man United haina hofu

Meneja wa Manchester United Sir Alex Ferguson amesisitiza timu yake haitaingiwa na hofu kubwa baada ya kuchapwa mabao 3-0 na Newcastle.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Ferguson asema hawana haja ya kuwa na hofu kubwa

Kufungwa kwa Manchester United mara ya pili katika muda wa siku tano, kumekuja baada ya kipigo cha kushangaza nyumbani kwao cha mabao 3-2 dhidi ya Blackburn.

"Tuna uzoefu wa kukabiliana na hali hiyo, tunahitaji kurejea vizuri uwanjani kwa kiwango chetu," alisema Ferguson, ambaye timu yake ipo nyuma kwa pointi tatu dhdi ya wanaoongoza ligi Manchester City.

"Huu si muda wa kuingiwa na hofu kubwa. Kupoteza mchezo kipindi kama hiki cha mwaka huwa inatokea katika baadhi ya nyakati."

Ferguson amekiri Manchester City sasa ndio wanashikilia uskukani wa Ligi Kuu ya England. Kikosi hicho cha Roberto Mancini kimefikisha pointi 48 baada ya kuilaza Liverpool mabao 3-0 siku ya Jumanne.

Manchester United pia watakuwa wanawasiwasi na Tottenham inayoshikilia nafasi ya tatu, ambao baada ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya West Brom, kumewaweka pointi tatu nyuma ya United.

Tottenham wataweza kufikisha pointi sawa na Manchester United iwapo watashinda mchezo wao dhidi ya Everton wiki ijayo.

Newcastle walipata bao la kuongoza kupitia kwa mpachika mabao wao hatari Demba Ba, kabla Yohan Cabaye kuongeza bao la pili kwa mkwaju maridadi wa adhabu ndogo.

Bao la tatu la Manchester United lilikuwa la kujifunga wenyewe baada ya Phil Jones kurudisha mpira langoni kwake na kumpoteza mlinda mlango wake.