Messi mchezaji bora 2011

Imebadilishwa: 9 Januari, 2012 - Saa 20:38 GMT
Messi

Messi apata tuzo hiyo mara ta tatu

Lionel Messi ameshinda tuzo ya Fifa ya mwanasoka bora wa mwaka 2011 ya Ballon d'Or, na kuwa mchezaji wa nne katika historia duniani kushinda tuzo hiyo mara tatu.

Mshambuliaji huyo kutoka Argentina mwenye umri wa miaka 24, aliwshinda Cristiano Ronaldo wa Real Madrid na mchezaji mwenzake wa Barcelona, Xavi.

Kocha wa Manchester United Sir Alex Ferguson alishinda tuzo ya huduma kwa soka, huku meneja wa Messi, Pep Guardiola akipata tuzo ya kocha bora wa mwaka.

Fergie

Sir Alex Ferguson naye ametunukiwa

"Nadhani Messi atavunja rekodi zote zilizopo," amesema Xavi.

Messi, ambaye aliwahi pia kushinda tuzo hiyo yenye hadi mwaka 2009 na 2010, alikuwa mchezaji bora katika mechi ya fainali ya Klabu Bingwa Ulaya mwaka 2011, dhidi ya Manchester United, na pia alishinda ligi ya Uhispania, kombe la Supercopa la Uhispania, Kombe la Uefa Duper Cup na Kombe la Dunia la klabu mwaka jana.

MESSI DHIDI YA RONALDO KATIKA LIGI NA ULAYA

  • MESSI

    MECHI: 47; MAGOLI: 43
  • RONALDO

    MECHI:44; MAGOLI: 48

Johan Cryuff na Marco van Basten wa Uholanzi, pamoja na Mfaransa Michel Platini, ndio wachezaji wengine waliowahi kushinda tuzo hiyo mara tatu.

"Ni furaha sana kwangu," alisema Messi. "Hii ni mara ya tatu ninashinda. Ni heshima ya kipekee. Nataka kuwashukuru kila mtu ambaye alihusika nami - wachezaji wenzangu, walimu wangu, madaktari, kocha na kila mmoja Barcelona.

Xavi

Messi akiwa na Xavi

"Pia ningependa kuishukuru timu ya taifa ya Argentina pia."

Mchezaji mwenzake Xavi alimiminia sifa akisema: "Bado kijana, ana miaka 24 tu. Atakuwa mmoja wa wachezaji wazuri zaidi katika historia ya mchezo huu."

Ferguson mwenye umri wa miaka 70, alipatiwa tuzo yake na Sepp Blatter ambaye alisema: "Soka zuri ni matokeo na kushinda, na hakuna anayeweza kufanya hivyo kama yeye."

Ferguson naye aliimwagia sifa Manchester United kwa kushirikiana naye katika mtazamo wake kwenye mchezo.

Alisema: Nimekuwa meneja mwenye na bahati sana kuweza kuwa na wachezaji wazuri ambao wameweza kufuata mtazamo wangu na ari niliyonayo, na hicho ndicho kinaifanya Manchester United kuwa klabu ya kipekee.

Wanashikilia ari ya kucheza, na ari ya kujaribu na kushinda."

Tuzo nyingine zilikwenda kwa nahodha wa timu ya taifa ya wanawake ya Japan iliyoshinda Kombe la Dunia, Homare Sawa. Meneja wa timu ya tifa ya Japan ya wanawake Norio sasaki; na Chama cha soka cha Japan kilipatiwa tuzo ya Fifa ya uchezaji wa haki huku mshambuliaji kutoka Brazil, Neymar, 19, anayechezea Santos akipata tuzo ya Fifa ya goli bora la mwaka 2011.

Taarifa zinazohusiana

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.