Manchester na Liverpool

Manchester United Haki miliki ya picha AFP
Image caption Welbeck na Rooney wafungaji

Katika michuano ya Kombe la FA Manchester United imeiondoa klabu bingwa iliyokua ikishikilia Kombe la FA Manchester City 3-2 na hivyo kuikwamisha kwenye hatua ya tatu ya michuano hii kwenye uwanja wa Etihad. Wayne Rooney alifunga mawili, moja likiwa la mkwaju wa peneti.

Bao la Wayne Rooney. Ikumbukwe kua Man.City ilicheza kwa kipindi kirefu bila nahodha wake Vincent Kompany aliyeondolewa kwa kadi nyekundu kwa kosa ambalo ilikua vigumu kulielezea.

Danny Wellbeck aliandika la tatu kuipa klabu yake matatu kwa bwerere kabla ya kipenga cha mapumziko. Kipindi cha pili Manchester City ilibadili mfumo wake kwa kutumia washambuliaji wawili badala ya mmoja Sergio Kun Aguero ambaye kipindi cha kwanza alizidiwa na mara hii akitegeme kiungo kilichoimarishwa.

Kufuatia kosa karibu na eneo la hatari kipindi cha pili kiungo Aleksandar Kolarov alikunja shuti iliyompita golkipa wa United na kuzitikiza nyavu kuhesabu bao la kwanza la City.

Timu ya watu kumi ya Man.City ilizidi kuishinikiza United na mnamo dakika ya 65 Sergio Aguero kupata la pili kufuatia kosa la mkongwe Paul Scholes aliyekubali kuichezea klabu yake miezi michache baada ya kutangaza kustaafu soka. Mcheza kiungo huyo ameitikia kiliyo cha Sir Alex Ferguson anayekabiliwa na majeruhi wengi msimu huu.

Manchester City ilijitahidi kutafuta bao la ushindi na Kolarov alikaribia kurudisha bao lakini United ikaponyoka na ushindi wa 3-2 ugenini, zawadi kubwa kuwaondoa mabingwa watetezi wa Kombe la FA.

Huku nyuma klabu ya Manchester City inasema kua itaomba rufaa kwa kadi nyekundu aliyoonyeshwa nahodha Vincent Kompany, kwa mujibu wa Kocha Roberto Mancini.

Mbali na michuano ya jumapili, Timu nyingine zilizovuka hatua ya tatu ni Liverpool iliyoinyunyizia klabu ya daraja la chini Oldham 5-1 siku ya ijumaa na jana jumamosi Swansea ikaibugiza Barnsley 4-2, Birmingham 0-0 Wolves,

Bristol Rovers 1-3 Aston Villa ,Everton 2-0 Tamworth, Fulham 4-0 Charlton, Gillingham 1-3 Stoke, Macclesfield 2-2 Bolton, MK Dons 1-1 QPR matokeo yaliyopelekea tetesi kwamba huenda wamiliki wa klabu hii ya QPR wameanza kutafakari Kocha mwingine badala ya Neil Warnock.

Newcastle ikazidi kumchafulia mambo kocha wa Blackburn kwa kuibugiza mawili kwa moja, Norwich city haikutaka mchezo kwa kuikandika Burnley 4-1.

Wigan inayoiwakilisha England katika michuano ya Ulaya ilitwikwa 2-1 na Swindon wakati Tottenham ikiichapa Cheltenham 3-0.

West Brom ikaifurusha Cardiff 4-2. Chelsea iliingia uwanja baada ya derby ya Manchester na hadi mapumziko Chelsea 0 Portsmouth, Lakini Klabu ya Ligi kuu ilionyesha makali yake kipindi cha pili kwa bao la J-Huan Matta mnamo dakika ya 48, Ramires akafuata na mawili kabla ya Frank Lampard kuhitimisha la dakika ya 93 ya majeruhi kwa la nne kuiweka Chelsea katika hatua ya nne.

Sunderland iliyocheza ugenini ilipewa mtihani hadi kipindi cha kwanza kuisha sufuri sufuri hadi Larsson kupachika la kwanza na dakika kumi baadaye McLean akatikisa nyavu za Peterborough.

Hadi mwisho Sunderland ikamaliza kwa kupiga hatua kushiriki hatua ya nne. West ham ikitarajia kuwazawadia mashabiki wake furaha ya mwaka mpya imeondolewa katika kinyanganyiro cha Kombe la FA kwa bao la dakika ya 88 la Sheffield wednesday. Kufuatia michuano ya Jumapili ilifanywa droo kupanga vilabu vitakavyoshiriki hatua ya nne.

Habari kuu za droo ni kwamba Liverpool imepangiwa kuchuana na Manchester United katika hatua ya nne ya Kombe la FA mchuano utakaofanyika uwanja wa Liverpool wa Anfield.

Nyingine ni mshindi wa pambano kati ya Brighton/Wrexham kuchuana na Newcastle, Sunderland izipige na Middlesbrough, mshindi wa Dagenham & Redbridge na Millwall atachuana na Southampton, Hull ichapane na Crawley, Chelsea ipambane na mshindi kati ya MK Dons au QPR, West Brom ichuane na Norwic, Mshindi wa pambano kati ya Leeds na Arsenal hapo kesho apambane na Aston Villa, Everton na Fulham, Derby v Stoke, Everton v Fulham.

Mechi hizi zitafanyika kati ya tarehe 28 na 29 mwezi huu.