Mtu wa "miujiza" kwa Khan si afisa IBF

Shirikisho la mchezo wa ngumi la Kimataifa - IBF limethibitisha "mtu wa miujiza" anayetuhumiwa na Amir Khan kwa kuingilia kadi za matokeo zinazoandikwa na majaji wakati alipochapwa na Lamont Peterson si afisa wao.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Mtu wa ajabuajabu pambano la Khan si wa IBF

Shirikisho hilo la ngumi limesema Mustafa Ameen si mwajiriwa wala hakupewa maagizo yoyote ya kufanya kazi kwa niaba ya IBF kama ilivyodaiwa na mmoja wa waandalizi wa pambano hilo.

Maelezo hayo ya IBF yanathibitisha madai yaliyotolewa na Khan, Freddie Roach, kwamba Ameen si afisa wa shirikisho la ngumi.

IBF imesema Ameen hakulipwa kwa kazi aliyoifanya na Sarb, ambayo ilikuwa kuwasaidia kwa fedha mabondia wastaafu wanaokabiliwa na matatizo.

Shirikisho hilo na ngumi limeamua kuvunja ukimya na kutoa uthibitisho wa kuwepo kwake Ameen nje ya ulingo wakati wa pambano ambapo ilionekana Khan alishindwa kwa uamuzi uliokuwa na utata na Peterson mjini Washington DC mwezi ulipita.

Taarifa hiyo imeongeza: "Bw Ameen alikubali kwamba atafanya kazi ya kuratibu kwa niaba ya shirikisho kwa malengo ya kuwaunganisha mabondia wastaafu ili IBF iwapatie msaada wa fedha.

"Bw Ameen si mfanyakazi au afisa wa shirikisho na wala hapokei fidia yoyote kutoka katika shirikisho hilo kutokana na jitahada zake anazofanya."

Taarifa hiyo ya IBF sasa itaongeza uzito kwa madai ya kambi ya Khan wanaotaka pambano lake dhidi ya Peterson litangazwe halikuwa la kuwania mkanda na wapewe nafasi ya mpambano huo urudiwe.

Iwapo hatua hiyo itaafikiwa basi Khan ataweza kurejeshewa mkanda wake.

Rufaa ya Khan itasikilizwa tarehe 18 mwezi wa Januari huko Newark, New Jersey.