Ivory Coast yaichapa Tunisia 2-0

Drogba Haki miliki ya picha Getty
Image caption Drogba na Kalou wote walifunga

Ivory Coast imeichapa Tunisia 2-0 katika mchezo wa kirafiki uliochezwa Abu Dhabi.

Mshambuliaji wa Chelsea Salomon Kalou alipachika bao la kwanza muda mfupi kabla ya mapumziko.

Dakika tatu baada ya mapumziko, Didier Drogba alifunga kwa mkwaju wa penati baada ya beki wa Tunisia Karim Hagui kuushika mpira ndani ya boksi.

Timu hizo mbili zimetumia mchezo huu kujianda na michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika 2012.

Baada ya dakika 73, Cheick Tiote wa Ivory Coast alitolewa kwa kadi nyekundu, baada ya kumchezea rafu Medji Traore.

Mshambuliaji Issam Jemaa wa Tunisia hakuweza kucheza kwa kuwa bado ni majeruhi.

Tunisia - ambao walishinda Kombe la Mataifa ya Afrika 2004 - watapambana na Morocco, Niger, na wenyeji Gabon katika kundi C.

Ivory Coast ambao wanadhaniwa kuwa na nafasi kubwa ya kuchukua kombe, watakuwa kundi B kupambana na Angola, Burkina Faso na Sudan.

Michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika inanza Equatorial Guinea Februari 21, huku fainali ikichezwa katika mji mkuu wa Gabon, Libreville Februari 12.