Bolt kushiriki mbio za Oslo

Bolt Haki miliki ya picha Getty
Image caption Usain Bolt kutimua vumbi Norway

Usain Bolt atajitokeza kwa mara ya kwanza katika mbio za kimataifa nwaka 2012 wakati atakaposhiriki michuano ya Bislett mjini Oslo Juni 7.

Bingwa huyo mara tatu wa dunia atashiriki katika mbio za mita 100 katika michuano hiyo, ambayo itafanyika wiki sita kabla ya michuano ya Olimpiki ya London 2012 kuanza.

Kabla ya hapo anapanga kukimbia mbio za majaribio na kujiandaa nchini Jamaica kuanzia mwezi ujao.

"Matayarisho yangu yamekuwa mazuri, mwaka 2012 utakuwa mwaka mzuri!" amesema kupitia taarifa.

"Sija majeraha, na ninafanya mazoezi makali na kila kitu kinakwenda kama kilivyopangwa".

Bolt, ambaye kwa sasa ni bingwa wa dunia anayeshikilia rekodi ya mbio za mita 100 na 200, atashiriki katika michuano ya mjini Kingston ya Camperdown Classi Februari 11, na tarehe 25 mwezi huo katika mbio za Gibson Relays na pia UWI International Machi 17.

Aidha anatarajiwa pia kushiriki mbio za mita 400 katika matayarisho kupima uwezo wake, huku mbio za kwanza akitarajiwa kushiriki michuano ya Jamaica International Invitational mjini Kingston tarehe 5 Mei.