Equatorial Guinea na Libya

Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika yanaanza wikendi hii, mechi ya ufunguzi ikichezewa Bata kati ya waandalizi Equatorial Guinea (wakishirikiana na Gabon) dhidi ya Libya.

Image caption Equatorial Guinea na Libya kufungua dimba

Bila shaka Libya itajaribu kuonyesha picha mpya, kufuatia mabadiliko ya kisiasa.

Libya iliwashangaza wengi ilipofuzu kuingia katika mashindano hayo, baada ya kutofungana mabao (0-0) ilipocheza na Zambia.

Hii nafasi kwa timu ya Libya kuanza upya, na baada ya kuitupa bendera yake iliyokuwa na msitari wa kijani kibichi, na kuanza kutumia iliyo na rengi nyekundu na nyeupe, na kuipatia timu jina jipya la Mediterranean Knights.

Hakuna anayeweza kusema kwamba maandalizi ya michuano hii ni kazi rahisi.

Ingawa Equatorial Guinea na Gabon ni mataifa jirani, kiutamaduni na kisiasa yana tofauti kubwa.

Equatorial Guinea ni taifa ambalo limeongozwa na Teodoro Obiang, ambaye ni kati ya marais wa Afrika ambao wamekuwa madarakani kwa muda mrefu sana barani Afrika.

Kifedha, ni taifa ambalo linanawiri kutokana na utajiri wake mkubwa kwa kutoa mafuta.

Hata hivyo, nchi hiyo inalaumiwa na wengi kwa kukosa uhuru wa kujielezea, na kwa kutozingatia haki mbalimbali za binadamu.

Nchini Gabon, rais Ali Bongo ndio tu ameweza kuwa imara zaidi, baada ya kupata kuungwa mkono na wengi katika bunge la nchi hiyo, kufuatia uchaguzi wa mwezi Desemba, ambao baadhi ya viongozi wa upinzani walitaka ususiwe.

Lugha ya taifa nchini Gabon ni kifaransa, lakini kihispania kunazungumzwa Equatorial Guinea.

Miji itakayochezewa mechi iko mbalimbali, na baya zaidi, mji mkuu wa Equatorial Guinea, Malaba, upo katika kisiwa cha Bioko, karibu na Cameroon.

Mashirika mapya ya vyombo vya habari yamechukizwa na ukiritimba na ugumu katika kupata vibali vya kuingia nchini humo na kutangaza moja kwa moja mechi zitakazochezwa katika mataifa hayo.

Vile vile kuna wasiwasi hali ya usalama itakuwa vipi, katika kuwapokea mamia ya waandishi wa habari, na vikundi mbalimbali vya wafanyikazi wa mashirika ya redio na televisheni.

Mashabiki wa soka barani Afrika wanauhusudu sana kandanda.

Lakini ni wangapi watasafiri, kwa mfano, kutoka Zambia hadi Bata?

Hata hivyo, licha ya matatizo ya usafiri, kuna matumaini kwamba michuano itakuwa ya kuvutia, na mataifa kama Niger na Botswana, yaliyofuzu kushiriki kwa mara ya kwanza, yataonyesha mchezo wa kusisimua.

Wengi wataitazama Niger, hasa kwa kuwa majirani Nigeria walishindwa kufuzu; lakini watapambana na ushindani mkali kutoka kwa Gabon, Tunisia na vile vile Morocco.

Muhimu pia katika mashindano haya ni suala la ni nani hayupo.

Sio tu Nigeria, lakini miamba mingine ya soka, Afrika Kusini, Cameroon na wachezaji hodari wa Misri, wote walishindwa kufuzu.

Je, kukosekana kwao kutakuwa na athari gani katika ubora wa mechi zitakazochezwa?

Ama labda mashabiki wengi watayageuzi mashindano kisogo kwa kukosekana miamba hiyo?

Lakini pasipo majina hayo makubwa, hii ni nafasi kwa wageni pia kuondoka na kombe.

Ivory Coast wanatazamiwa na wengi kuondoka na ushindi, lakini mataifa ya Ghana na Senegal pia yana nafasi nzuri.

Kutokuwepo kwa Misri ni matumaini kwa mabingwa hapo zamani, Morocco au Tunisia, kutazamiwa na mashabiki wa Afrika ya Kaskazini kulifikisha kombe huko.