Wenger awajia juu mashabiki wa Arsenal

Meneja wa Arsenal Arsene Wenger, ametetea uamuzi wake wa kumpumzisha Alex Oxlade-Chamberlain na nafasi yake kuchukuliwa na Andrey Arshavin wakati walipolazwa mabao 2-1 na Manchester United.

Image caption Wenger ajitetea kwa nini alimbadilisha Oxlade-Chambelain

Baadhi ya mashabiki wa Arsenal walisikika wakizomea wakati Oxlade-Chamberlain, aliyekuwa chachu ya kupatikana bao la kusawazisha la Arsenal, alipompatia pasi nzuri mfungaji Robin van Persie alipopumzishwa.

"Nimekuwa meneja kwa miaka 30 na nimeshabadilisha wachezaji mara 50,000. Siwajibiki kueleza sababu za kumpumzisha mchezaji kwa mtu yeyote," alisema.

Arsenal iko nyuma ya Chelsea wanaoshilikia nafasi ya nne kwa pointi tano katika mbio za kuwania kufuzu kwa ajili ya kuwania Ubingwa wa Ulaya msimu ujao.

Oxlade-Chamberlain alikuwa mmoja wa wachezaji waliong'ara kwa Arsenal katika mtanange huo uliochezwa katika uwanja wa Emirates.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 18, ilikuwa ni mara yake ya kwanza kuanza kucheza mechi yake ya Ligi Kuu ya England, alikuwa akimlisha sana mipira Van Persie wakati wa kipindi cha pili ambapo Arsenal walionekana kucharuka.

"Naelewa mashabiki wamechukizwa kutokana na kumbadilisha Oxlade-Chamberlain, hasa baada ya mabadiliko hayo yaliposhindwa kuzaa matunda, lakini alianza kuchoka," Wenger alifahamisha kutokana na uamuzi wake wa kumpumzisha winga huyo wa zamani wa Southampton.

"Wiki hii alikuwa akiumwa. Arshavin ni nahodha wa timu ya taifa ya Urusi. Una kijana mwenye umri wa miaka 18 akiwa ndio anaanza kwa mara ya kwanza mechi ya Ligi Kuu na mchezaji ambaye ni nahodha wa timu ya taifa ya nchi yake na watu wanahoji kwa nini nimefanya mabadiliko hayo?"

Alipoulizwa namna kufungwa huko kulivyoiathiri timu yake, Wenger alisema ilikuwa ni mechi ya Arsenal "ambayo isingepaswa kupoteza" kabla ya kuongeza: "Imetuweka katika nafasi ngumu sana."

Meneja wa Manchester United Sir Alex Ferguson alisema kikosi chake kilistahili kushinda hali iliyowaweka pointi tatu nyuma ya Manchester City wanaoongoza ligi kwa sasa.

"Hatimaye nilihisi kikosi chetu kilikuwa imara," alisema. "Hongera kwa wachezaji nafasi ya ulinzi, ambao walifanya kazi kubwa.

Alipoulizwa juu ya kuikamata Manchester City, alisema: "Itakuwa ni kibarua kigumu kwetu sote."