Wakala asema Balotelli anahisi anaonewa

Wakala wa Mario Balotelli ameonya mshambuliaji huyo anaweza kuachana na kandanda ya England iwapo ataendelea kama aonavyo hatendewi haki .

Haki miliki ya picha PA
Image caption Wakala wa Balotelli aonya mchezaji huyo ataondoka England

Balotelli, anakabiliwa na adhabu ya kutocheza michezo minne baada ya kushtakiwa na Chama cha Kandanda cha England kwa kitendo cha vurugu.

Mshambuliaji huyo wa Manchester City alionekana kumkanyaga kichwani Scott Parker kabla ya kufunga bao la ushindi kwa mkwaju wa penalti na kuipatia ushindi Manchester City wa mabao 3-2 dhidi ya Tottenhamon siku ya Jumapili.

"Nadhani anahisi anateswa; hawezi kuendelea namna hii," alisema Mino Raiola.

Wakala Raiola aliongeza alipokuwa akihojiwa moja kwa moja na BBC Radio 5: "Tulikuwa na mtazamo uliokuwa wazi tangu mwanzo kutokana na kazi yake ya kusakata kandanda na niliwaambia waandishi wa habari wazi kwamba Mario ataichezea Manchester City kwa takriban miaka mitatu hadi minne, kwa kuisaidia klabu katika kipindi hiki muhimu na akiwa mchezaji na mwanaume.

Bila shaka yoyote iwapo atafungiwa kucheza mechi tatu au nne kwa sababu moja au nyingine, hatutaweza kwenda namna hii na kuna haja ya kufikia mwisho katika mambo hayo.

"Kwa hiyo kama mambo yapo namna hiyo na waamuzi wa Kiingereza pamoja na Chama cha Soka-FA watataka Mario aondoke England basi tutalichukulia kwa makini suala hilo, pamoja na kwamba hiyo haikuwa si nia yetu.

"Mario amesikitishwa sana na uamuzi huo. Anapenda kucheza England. Amekuwa akihoji "kwa nini kila mara mimi, kwa nini kila mara jambo linanitokea mimi? Anapenda kucheza kandanda England na nadhani anahisi anateswa.

Alijiunga na Manchester City mwaka 2010 akitokea Inter Milan kwa kitita cha paundi milioni 24 lakini amekuwa katikati ya mizozo kadha ndani na nje ya uwanja.

Tangu aanze kucheza kandanda England ameshatolewa nje kwa kadi nyekundu mara tatu, hakuweza kuendelea kucheza baada ya mwili wake kutopatana na nyasi za Kiev, alimrushia mshale wa kuchezea mchezo wa dart mchezaji mmoja wa timu ya akiba na alinusurika kujeruhiwa baada ya kutokea mlipuko wa fashifashi iliyolipuka nyumbani kwake.