Ghana yashinda, Mali nayo yaanza vizuri

Ghana imeanza kampeni yake ya kulisaka Kombe la Mataifa ya Afrika kwa ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya wanagenzi Botswana.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Ghana walipopambana na Botswana

Nahodha John Mensah aliipatia Black Stars bao hilo moja kipindi cha kwanza, alipotumbukiza mpira wa kona wavuni akiwa karibu kabisa na lango.

Lakini nahodha huyo alisababisha atolewe nje kwa kadi nyekundu baada ya kumuangusha mshambuliaji wa Botswana Jerome Ramatlhakwane, wakati akielekea kupachika bao.

Ghana ilimiliki mpira kwa sehemu kubwa ya mchezo, lakini iliambulia ushindi mwembamba, ingawa baada ya kutolewa kwa Mensah kipindi cha pili,Botswana walionekana kucharuka na kuwafanya Ghana wacheze zaidi eneo la kati.

Mali imeungana na Ghana kileleni katika kundi D baada ya kuilaza Guinea 1-0 katika mtanange uliokuwa wa vuta nikuvute katika mji wa Franceville.

Haki miliki ya picha
Image caption Kikosi cha Mali katika mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika

Bakaye Traore alifunga bao hilo pekee katika dadika ya 30 kwa mkwaju mkali uliomgonga mlinda mlango wa Guinea Naby Yattara.

Guinea walikuwa tishio kubwa kupitia washambuliaji hatari chipukizi Alhassane Bangoura, Ibrahima Diallo na Ismael Bangoura lakini walishindwa kuipenya ngome imara ya Mali.

Wanaoongoza katika kundi D ni Mali na Ghana, ambao mapema waliwalaza Botswana bao 1-0.

Baada ya mchezo huo wa mwisho baina ya Mali na Guinea sasa timu zote 16 zimeshacheza katika mashindano ya mwaka huu ya Kombe la Mataifa ya Afrika huku kila mchezo kumepatikana mshindi.