Tevez aingia hasara ya paundi milioni 9

Mzozo baina ya Carlos Tevez na Manchester City umemgharimu mshambuliaji huyo wa Argentina paundi milioni 9.3 za mshahara wake, faini alizotozwa na kupoteza bakhshishi.

Haki miliki ya picha PA
Image caption Mzozo wa Tevez wamgharimu mchezaji huyo paundi milioni 9

Imefahamika hajalipwa mshahara wake, unaokadiriwa kuwa paundi 200,000 kwa wiki, tangu mwishoni mwa mwezi wa Novemba.

Na pia hivi majuzi alitozwa faini ya paundi milioni 1.2 kwa utovu wa nidhamu baada ya kukataa kurejea akitokea Amerika Kusini.

Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Manchester City Khaldoon al-Mubarak aliishutumu klabu ya AC Milan kutokana na mwenendo wao kujaribu kumsajili Tevez, akisema mbio za kumchukua zinawashinda.

Tevez mwenyewe anapendelea kujiunga na AC Milan lakini Al-Mubarak aliishutumu klabu na makamu mwenyekiti wa AC Milan Adriano Galliani, akisema Wataliano hao mazungumzo yao na Tevez pamoja na washauri wake yalikuwa ya "haraka".

"Kadri mambo yanavyokwenda, AC Milan si chaguo la Carlos," alisema Al-Mubarak, ambaye atakuwa tayari kumuachia Tevez kwa kitita cha paundi milioni 25.

Akizungumza kwa mara ya kwanza hadharani, Al-Mubarak aliliambia gazeti la Abu Dhabi: "Iwapo wanataka tuwasikilize wakati huu wa dirisha dogo la usajili, wanawajibika kuacha mara moja kupongezana na waanze kufikiria namna watakavyokubaliana na matakwa yetu.

Mzozo huu unaoendelea ulianza wakati Tevez alipotozwa faini ya kukatwa mshahara wa wiki mbili baada ya meneja Roberto Mancini kudai mshambuliaji huyo alikataa kucheza akiwa mchezaji wa akiba wakati Manchester City walipopambana na Bayern Munich mwezi wa Septemba katika patashika za Ubingwa wa Ulaya, ingawa Tevez alidai hawakuelewana.

Alikwenda Amerika Kusini na kugoma kwake kurejea kumemsababishia atozwe faini ya kukatwa mshahara wa wiki sita ambao ni sawa na paundi milioni 1.2.

Mkataba wa sasa wa Tevez unamalizika mwezi wa Juni mwaka 2014, lakini mshambuliaji huyo hajacheza kandanda tangu tarehe 21 mwezi wa Septemba na kwa sasa yupo kwao Argentina.