Ivory Coast yaingia robo fainali

Ivory Coast ilifanikiwa kuishinda Burkina Faso 2-0 katika uwanja wa Malabo na kufuzu kuingia robo fainali ya michuano ya Kombe la Mataifa barani Afrika.

Haki miliki ya picha
Image caption Salomon Kalou alifunga bao la kwanza la Ivory Coast

Mshambulizi wa klabu ya Chelsea ya England, Salomon Kalou, ndiye aliyeanza kuona wavu kwa kufunga bao la kwanza katika dakika ya 16, na Bakary Kone akamfunga kipa wake mwenyewe, zikiwa zimesalia dakika nane kabla ya mechi hiyo kumalizika.

Lakini licha ya wachezaji wengi wa Ivory Coast ambao huwa wanacheza katika ligi kuu ya Premier nchini England kuwa uwanjanji, hawakuonyesha mchezo wa kusisimua, kwani wachezaji wa Burkina Faso waliweza kuumiliki mpira kwa muda mrefu.

Kwa kushindwa katika mechi mbili mfululizo, juhudi za Burkina Faso hazikufika popote, na itabidi kurudi nyumbani.

Katika mechi iliyotangulia Alhamisi, Sudan iliweza kupata pointi yake ya kwanza katika mashindano hayo, baada ya miaka 36, kufuatia sare ya 2-2 ilipocheza na Angola.

Mechi hiyo pia ilichezewa mjini Malabo.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Sudan ilijikakamua na kutoka sare na Angola

Angola iliweza kupata bao la kwanza, baada ya dakika nne tu, wakati Manucho alipogundua kosa lililofanywa na washambulizi wa Sudan, na kwa haraka akaitumia nafasi iliyojitokeza kuandikisha bao.

Lakini baada ya juhudi kubwa, Sudan iliandikisha bao lake la kwanza katika fainali za mashindano hayo, tangu mwaka 1976, wakati Ahmed Bashir aliingiza wavuni bao la kichwa.

Manucho alifunga tena kwa mkwaju wa penalti, lakini naye Bashir akapata bao la kusawazisha, katika dakika za mwishomwisho za mchezo.

Mechi za Ijumaa zitachezewa katika uwanja wa Libreville, wakati Gabon, ambao wanashirikiana na Equatorial Guinea kuandaa mashindano, watawakaribisha Morocco.

Hii inatarajiwa kuwa mechi ngumu na ya kusisimua.

Hata hivyo, kabla ya mechi hiyo, Niger, ambayo inashiriki katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa mara ya kwanza, itapambana na Tunisia.