Kati ya wale waliohama

Louis Saha Haki miliki ya picha 1
Image caption Saha anaondoka kuelekea Tottenham katika usiku ambao timu yake ya awali Everton imeishinda Man City

Muda uliowekwa wa kufungwa kwa dirisha la usajili ulitimia Jumanne, saa tano usiku za Uingereza, na baadhi ya wachezaji watakaohama kutoka vilabu vyao ni pamoja na mshambulizi wa Everton, Louis Saha.

Saha anaelekea Tottenham kwa mkopo, awali kwa miezi sita, yaani hadi mwisho wa msimu, lakini baada ya hapo, mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 33 atakuwa na uhuru wa kupata mkataba wa kudumu.

Everton imemchukua tena mchezaji wake wa zamani, Steven Pienaar, kwa mkopo kutoka Tottenham.

Wakati huohuo Everton pia imemnyakua Nikica Jelavic kutoka klabu ya Uskochi, Rangers, kwa pauni milioni 5.5.

Meneja wa West Brom, Roy Hodgson naye amempata kiungo cha kati wa Jamhuri ya Ireland, na ambaye alikuwa mchezaji wa Blackburn, Keith Andrews.

Hodgson amesema; "Keith ni mchezaji ninayemfahamu vizuri, na amenivutia kwa miaka michache".

"Ataleta ujuzi mkubwa katika timu, na ana rekodi nzuri pia ya kufunga mabao", alielezea.

Wolves nao wamemchukua mchezaji Sebastien Basson, mwenye umri wa miaka 25, kwa mkopo kutoka Tottenham.

West Ham ilifanikiwa pia kukamilisha utaratibu wa kumsajili Ravel Morrison kutoka Manchester United, na Nicky Maynard kutoka Bristol City.

Swansea nayo imempa mkataba wa miaka mitatu na nusu kijana mwenye umri wa miaka 22, Curtis Obeng, kutoka Wrexham.

Yeye hucheza ulinzi, upande wa kulia.

Meneja wa QPR, Mark Hughes naye ametumia pauni milioni 4 kumsajili Bobby Zamora, kutoka kwa klabu aliyoifundisha zamani ya Fulham.

Hughes amefurahia sana kumpata pia mshambulizi wa zamani wa Liverpool na vile vile Sunderland, Djibril Cisse.

Anasema, "Djibril Cisse anaifahamu ligi ya Premier, na atatuongezea kasi na nguvu, mambo ambayo tumekuwa tukiyakosa".

Manchester City wametangaza kuwasili kwa kiungo cha kati kutoka Chile, David Pizarro, mwenye umri wa miaka 32, kwa mkopo pasipo malipo, hadi mwisho wa msimu.

Chelsea wamemsajili kijana kutoka Notttingham Forest, mshambulizi Patrick Bamford, kwa pauni milioni 1.5.

Bamford, kijana wa miaka 18, anajiunga na timu ya akiba ya Chelsea.

Manchester United imemsajili kijana wa miaka 19, mlinzi Frederic Veseli kutoka Uswisi, aliyekuwa akiwachezea majirani Manchester City.