Terry avuliwa unahodha wa England

John Terry amevuliwa unahodha
Image caption John Terry amevuliwa unahodha wa timu ya taifa ya England

Chama cha soka nchini Uingereza kimemvua John Terry unahodha wa timu ya taifa ya England.

Chama hicho cha soka kinasema Terry hapaswi kushika unahodha wa timu ya taifa hadi pale kesi inayomkabili ya madai ya kumtamkia matusi ya kibaguzi mchezaji mweusi mwaka jana.

John Terry amekanusha mashtaka hayo.

Hata hivyo chama cha soka Uingereza kimesema anaweza kubakia katika timu ya taifa.

Analaumiwa kwa kumtamkia matusi hayo mlinzi wa timu ya QPR Anton Ferdinand wakati wa mechi kati ya timu hiyo na Chelsea mwaka 2010.

Meneja wa timu ya taifa ya England Fabio Capello alikuwa amesisitiza kwamba atabakia kuwa nahodha wa timu hadi itakapothibitishwa kuwa ana hatia.

FA imesema imechukua uamuzi huo kwa sababu kesi hiyo itakuwa haijaanza wakati wa mashindano ya kombe la bara ulaya baadaye mwaka huu.

Terry amekwisha pokonywa unahodha katika siku zilizopita.

Aliondolewa kutoka nafasi hiyo mwaka 2010 kufuatia madai kwamba alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanamke mpenzi wa mchezaji mwenzake.