Capello ajiuzulu umeneja wa England

Capello amejiuzulu Haki miliki ya picha AFP
Image caption Fabio Capello amejiuzulu kama meneja wa timu ya taifa ya England

Fabio Capello amejiuzulu kama kocha wa timu ya taifa ya England, chama cha soka nchini humo kimethibitisha.

Kocha huyo kutoka Italia amejiuzulu baada ya kukutana na mwenyekiti wa chama cha soka England David Bernstain kujadili hatua ya chama hicho ya kumvua unahodha wa timu ya taifa mlinzi John Terry.

Terry alivuliwa unahodha hadi pale kesi inayomkabili mahakamani ya kumtamkia maneno ya kibaguzi mlinzi wa timu ya QPR Anton Ferdinand itakapomalizika.

'' Baada ya mkutano uliochukua zaidi ya saa moja uamuzi wa Bw Capello wa kujiuzulu ulikubaliwa na ataacha wadhifa wa meneja wa timu ya taifa mara moja." Taarifa ya chama cha soka England ilieleza.

Capello alizungumza kwenye Televisheni ya Italia akaelezea kupinga uamuzi wa chama cha soka England wa kumvua Terry unahodha.

Mlinzi wa Chelsea John Terry anakabiliwa na mashtaka mahakamani kufuatia madai kuwa alimtamkia Anton Ferdinand maneno ya kibaguzi wakati wa mechi kati ya Chelsea na QPR mwezi Oktoba mwaka uliopita.

Tayari vyombo vya habari Uingereza vinabashiri kwamba meneja wa timu ya Tottenham Hot Spurs Harry Rednapp atachukua wadhifa wa meneja wa timu ya taifa ya England.