Wolves wamtafuta meneja bora

Kulingana na mkurugenzi mkuu wa Wolves, Jez Moxey, wanamhitaji meneja mzoefu kurithi kazi ya Mick McCarthy.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Alifutwa kazi baada ya Wolves kushindwa 5-1 walipocheza na West Brom

McCarthy alifutwa kazi Jumatatu, mara tu baada ya timu ya Wolves kunyeshewa magoli 5-1, katika mechi ya Jumapili, licha ya kwamba Wolves walikuwa wakichezea uwanja wa nyumbani.

"Hii si kazi ya kurutu", ameelezea Moxey akizungumza na BBC.

"Lazima tufanye kazi haraka katika kuhakikisha tunampata meneja anayefaa, lakini katika mawazo yetu tutakuwa huru juu ya atakayeajiriwa, iwe ni kwa muda mfupi au kipindi kirefu".

Kwa mbwa mwitu kushindwa kubweka baada ya kipigo cha hivi karibuni, bado wamo katika hatari ya kuondolewa katika ligi ya Premier msimu huu.

Wolves wana mechi 13 zilizosalia kujitahidi kuepuka kushuka daraja na kujipata tena katika mechi za Championship.

McCarthy aliwasaidia kupandishwa daraja na walipofuzu kuingia ligi ya Premier mwaka 2009.

Steve Bruce, ambaye alifutwa kazi na klabu ya Sunderland mwezi Novemba, na Alan Curbishley, ambaye kazi yake kama meneja ilikwisha mwezi Septemba mwaka 2008 alipojiuzulu kama meneja wa West Ham, ni kati ya watu wanaozungumzwa kwamba huenda wakaajiriwa na Wolves.

"Tuna mashabiki wazuri sana, uwanja mzuri na historia ya kupendeza. Tumo katika ligi ya Premier, na tungelipenda kubakia katika ligi ya Premier, na kwa hiyo nadhani tuna mambo yanayoweza kumvutia meneja mzuri."

Moxey amekanusha McCarthy amefutwa kazi kufuatia matokeo mabaya ya Jumapili.

"Matokeo dhidi ya West Brom yalikuwa ni mabaya kwa wote, na ni sawa na msumari wa mwisho kutundikwa katika jeneza", alielezea.

"Lakini sababu sio kufungwa na West Brom. Ukweli ni kwamba tulikuwa na pointi 14 kutoka kwa mechi 22 zilizopita".

Moxley alijiunga na bodi ya Wolves mwezi Juni mwaka 2000, katika kipindi ambacho meneja Dave Jones na Glenn Hoddle walitoa mafunzo kwa wachezaji, kabla ya McCarthy kuajiriwa mwezi Julai mwaka 2006.