Matokeo ya Teknolojia yaridhisha

Wataalamu wa sheria za mchezo wa mpira wa miguu wameidhinisha mifumo miwili ya teknolojia inayoweza kusaidia katika uwamuzi wa kuthibitisha kama goli limevuka ule mstari.

Hata hivyo uwamuzi uliofikiwa itabidi usubiri hadi kikao kitakachofanywa mwezi Julai ambapo kura zitapigwa juu ya kama teknolojia hio itumike kuania mwaka 2014 kwenye fainali za Kombe la Dunia nchini Brazil.

Bodi ya Kimataifa inayohusika na masuala ya soka mapema leo ilichunguza na kutathmini matokeo ya mfumo uliozoweleka wa Hawk Eye katika mchezo wa Tennis na Marefa waliohudhuria wameonyesha kuridhika na majaribio yaliyofanyawa na kuelekea hatua ya pili ya majaribio.

Itakumbukwa kua Rais wa FIFA, Sepp Blatter mnamo siku ya Ijumaa alibadili msimamo wake wa mda mrefu wa kutoridhia mapendekezo ya kutumia teknolojia inayoweza kusaidia kuondoa ubishi wa kama goli limevuka mstari au la, mfano wa bao lililofungwa na mcheza kiungo wa England Frank Lampard dhidi ya Ujerumani kwenye fainali za Kombe la Dunia nchini Afrika ya kusini mwaka 2010.

Mkutano wa bodi ijulikanayo kama IFAB mwezi Julai pia utaamua kama wachezaji Waislamu waruhusiwe kucheza wakivalia Hijab kuambatana na sheria za dini ya Kiislamu. Hili ni kufuatia mapendekezo yaliyowasilishwa mbele ya kikao na Prince Ali ambaye ni Makamu Rais wa FIFA.