Fifa yaisafisha Afrika Kusini na rushwa

Mtaalam wa uchunguzi wa Fifa amesema matokeo ya awali uchunguzi wake kuhusiana na kupanga matokeo ya mechi za kimataifa, hakuweza kupata ushahidi wa kuihusisha Afrika Kusini.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Makao makuu ya Fifa

Mechi chache ilizocheza Bafana Bafana wakati wa kujiandaa kwa mashindano ya Kombe la Dunia mwaka 2010 zinachunguzwa, ikiwemo michezo miwili ya kirafiki dhidi ya Colombia na Guatemala.

Lakini mkuu wa usalama Chris Eaton amebainisha kwamba aliyekutwa na hatia ya kujihusisha na kupanga matokeo ya mechi Wilson Raj Perumal, alikishawishi Chama cha Kandanda cha Afrika Kusini kuwateua waamuzi kupitia kampuni yake.

Perumal kwa sasa yupo jela nchini Finland.

Raia huyo wa Singapore alihukumiwa kifungo cha miaka miwili jela mwezi wa Julai mwaka 2011 kutokana na kashfa ya kupanga matokeo ya mechi za ligi ya daraja la juu nchini Finland.

Perumal pia inaaminika alishiriki kwa kiasi kikubwa kupanga matokeo ya mechi za timu ya taifa ya Zimbabwe ilipofanya ziara katika bara la Asia, ambapo michezo kadha ya kimataifa matokeo yake yalipangwa, ingawa uchunguzi wa sasa umetuama zaidi kwa michezo iliyocheza timu ya Afrika Kusini muda mfupi kabla ya kuanza kwa mashindano ya Kombe la Dunia mwaka 2011.

Matokeo ya mechi za kirafiki dhidi ya Thailand, Colombia, Bulgaria na Guatemala wiki chache kabla ya kuanza kwa heka heka za Kombe la Dunia, zote zinachunguzwa baada ya Fifa kugundua waamuzi walitolewa na kampuni moja ya Singapore, vinara wa biashara ya upangaji matokeo ya mechi.

Mwezi wa Mei mwaka 2010, ukiwa mwezi mmoja kabla ya kuanza fainali za Kombe la Dunia, wenyeji Afrika Kusini walicheza na Colombia na kuwalaza mabao 2-1 na pia wakawacharaza Guatemala mabao 5-0 katika michezo miwili ya kirafiki ambapo katika mechi hizo kulipatikana mikwaju mitatu ya penalti.