Mtanange wa Manchester kuamua bingwa

Meneja wa Manchester City Roberto Mancini amesema ubingwa wa Ligi Kuu ya England utaamuliwa wakati kikosi chake kitakapokabiliana na Manchester United huku ikisalia michezo mitatu kabla ya kukamilika kwa ligi hiyo.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Roberto Mancini anaamini pambano na Man United litaamua bingwa

Kikosi cha Mancini kienguliwa katika uongozi wa ligi baada ya kuchapwa na Swansea na sasa wapo nyuma ya majirani zao kwa pointi moja.

Lakini Manchester City itaialika Manchester United katika uwanja wao wa Etihad tarehe 30 mwezi wa Aprili na Mancini anaamini mchezo huo ndio utaamua nani atakuwa bingwa msimu huu.

Wakati Machester City wakipoteza mchezo dhidi ya Swansea siku ya Jumapili kwa kulazwa bao 1-0, Manchester United walifanikiwa kuchupa na kukalia kiti cha uongozi baada ya ushindi wa mabao 2-0 siku hiyo ya Jumapili dhidi ya West Bromwich Albion, lakini Mancini anasema hana wasiwasi na kuenguliwa kutoka uongozi wa ligi wakati zikiwa zimesalia mechi 10 kabla ya msimu huu kumalizika.

Mancini bado anaamini Manchester City inaweza kunyakua ubingwa kwa mara ya kwanza baada ya miaka 44.

Mancini anaamini walistahili kupata angalao pointi katika mchezo wa Jumapili na akaongeza: "Tulikosa nafasi tatu au nne wakati tuliposhambulia kwa kushtukiza.

"Hilo ndio tatizo letu kwa wakati huu na tulifungwa bao la kijinga."

Meneja huyo wa Manchester City pia alitupilia mbali taarifa za kukwaruzana na kiungo wa England Gareth Barry, ambaye alitoleana maneno makali na meneja msaidizi David Platt wakati alipokuwa akitoka uwanjani baada ya kubadilishwa.

"Gareth alikuwa na matatizo kwa wiki tatu," alisema Mancini. "Gareth ana matatizo, sijui wapi ila ana jeraha dogo.

Alipoulizwa kukasirika kwa Barry baada ya kutolewa, Mancini alijibu: "Hiyo ni kawaida.Mimi ndiye ninayeamua. Mimi ndiye meneja."

Pia aliulizwa kuhusiana na taarifa kwamba mshambuliaji Mario Balotelli na kiungo Yaya Toure walizozana katika njia ya kuelekea vyumba vya kupumzikia wakati wa mapumziko, Mancini alijibu: "Sijui lolote."

Na kuhusiana na taarifa za sasa za Carlos Tevez, Mancini anaamini mshambuliaji huyo amebakiza siku 10 kabla ya kuwa tayari katika kikosi cha kwanza.