Muamba hali mahututi

Fabrice Muamba, kiungo cha kati katika klabu ya Bolton Wanderers, yumo katika hali mahututi baada ya kuzimia Jumamosi katika mechi ya raundi ya tano ya Kombe la FA dhidi ya Tottenham.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Muamba alizimia ghafula uwanjani.

Mchezaji huyo anaendelea kupata matibabu katika hospitali inayohusika zaidi na magonjwa ya kifua, London Chest Hospital.

Madaktari walijaribu kumsaidia kuvuta pumzi kwa kipindi cha dakika 10 mara tu alipozimia uwanjani, lakini hayo yaliposhindikana, ilibidi akimbizwe hospitali.

"Bolton Wanderers inathibitisha kwamba Fabrice Muamba amelazwa katika kituo cha mshituko wa moyo cha London Chest Hospital na akiwa katika hali mahututi", ilieleza taarifa ya pamoja iliyotolewa saa 2130 GMT Jumamosi kutoka kwa klabu ya Bolton na vile vile hopitali hiyo.

"Hakuna maelezo zaidi ambayo yatatolewa wakati huu. Klabu na vile vile hospitali vinatoa mwito kwa vyombo vya habari na umma kuiheshimu familia yake wakati huu na kuwapa nafasi katika kushughulika na suala hili".

Mechi hiyo ya Kombe la FA kati ya Tottenham na Bolton Wanderers ilisimamishwa ghafula baada ya Fabrice Muamba kuzimia ghafula.

Madaktari walijaribu kwa dakika 10 kumfanya mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 23 aweze kupumua, na hilo liliposhindikana, ilimlazimu mwamuzi Howard Webb kusimamisha mchezo.

Mwandishi wa BBC Radio 5, Ian Dennis, alielezea kwamba mchezaji huyo inaelekea alikuwa katika hali ya taabani.

Mchezo ulikuwa ni sare ya 1-1 wakati mechi iliposimamishwa katika dakika ya 41.

Muamba alizaliwa tarehe 6 Aprili mwaka 1988 mjini Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, na aliimarika kisoka katika chuo cha vijana wadogo cha Arsenal, na akiiwakilisha England katika mechi mbalimbali, tangu zile za vijana wa miaka 16, hadi zile za wale wa miaka 21.

Alijiunga na Birmingham mwaka 2007, na kuhamia Bolton mwaka uliofuata.

Muamba alicheza katika mechi za Ulaya mwaka 2011, za vijana wa chini ya umri wa miaka 21, akiichezea England katika mashindano yaliyofanyika nchini Denmark.

Wachezaji wenzake wa ligi ya Premier katika mitandao ya jamii wamekuwa wakimtakia nafuu.

"Tunakuombea Fab. Tunatumaini yuko salama. Mawazo yetu ni juu ya familia yako. Tunasubiri kwa matumaini habari zako kutoka kwa wenzetu. Fab ni mtu anayejizatiti!" aliandika kiungo cha kati wa Bolton, Stuart Holden.

"Tumuombee Fab. Kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu, atapona." aliandika mshambulizi wa Tottenham, Jermain Defoe