Ukame wa mabao sasa historia kwa Torres

Fernando Torres amesema maendeleo yaliyoonekana hivi karibuni katika timu yake ya Chelsea yamemsaidia kumaliza ukame wa mechi 24 bila kufunga bao.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Torres akishangilia na wenzake baada ya kufunga bao

Torres, aliyenunuliwa kwa kitita cha paundi milioni 50 mwezi wa Januari 2011, alifunga bao lake la kwanza tangu tarehe 19 mwezi wa Oktoba na akafunga jingine wakati Chelsea ilipoiadhibu Leicester mabao 5-2 katika robo fainali ya kuwania Kombe la FA.

"Nilikuwa nayahitaji mabao hayo. Nimekuwa nikifanya kazi ya ziada kuweza kuyapata," Torres alisema.

"Katika mwezi uliopita timu imeimarika. Tunajituma zaidi na tumeonesha katika michezo minne iliyopita tumenuia kumaliza msimu vizuri."

Chelsea hadi sasa imeshinda michezo minne mfululizo tangu Roberto di Matteo alipoteuliwa kuchukua nafasi ya meneja aliyetimuliwa mwezi uliopita Andre Villas-Boaslast.

Torres amedai kwa sasa anajihisi raha zaidi kucheza chini ya meneja wa muda Di Matteo, lakini akasisistiza amekuwa akiridhishwa na kiwango chake licha ya kukosa kufunga mabao.

"Huenda msimu huu nimekuwa nikicheza katika kiwango kizuri na bila kufunga mabao. Hiyo ndio kazi ya mshambuliaji na iwapo hufungi watu watakuwa wanafikiria unacheza ovyo," aliongeza.

"Lakini mashabiki, wenzako katika timu na wafanyakazi wengine wamekuwa wakiniunga mkono na najihisi mwenye raha kwa meneja wa sasa. Ni wakati mzuri kwa Chelsea.

"Tunacheza vizuri katika safu ya ulinzi na iwapo tutaendelea kutengeneza nafasi kama hizi nyingi, itakuwa kazi kuifunga Chelsea."

Di Matteo amebainisha kamwe alikuwa hana wasiwasi na kiwango cha Torres na alikuwa na matumaini mshambuliaji huyo atajirekebisha akiwa karibu na lango na kufunga.

Meneja huyo wa muda alihisi Torres alikuwa akikabiliwa na "matatizo ya kisaikolojia" lakini kila mara alikuwa mchezaji muhimu kwa timu.