Hamilton kuongoza mbio za Malaysia

Lewis Hamilton Haki miliki ya picha AFP
Image caption Lewis Hamilton

Kwa wiki ya pili mfululizo dereva wa Timu ya magari ya McLaren Lewis Hamilton ameongoza mbio za kufuzu kuchambua ni nani ataongoza katika kuanza mashindano jumapili akifuatiwa na mwenziye Jenson Button.

Michael Schumacher wa Mercedes kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka mitano na nusu ameweza kujikuta katika nafasi za mbele.

Washindi wa mbio hizi msimu uliopita Red Bull walijikuta katika nafasi mbovu baada ya dereva wao kiongozi Sebastian Vettel kuweza kushinda nafasi ya nne ingawa Mjerumani huyo amesema ana mpango wa jinsi ya kuipata nafasi ya mbele katika kumaliza mbio.

Bingwa huyo wa dunia alikua miongoni mwa viongozi waliofuzu kwa kutumia tairi ngumu jambo ambalo linaweza kumsaidia wakati wa mashindano jumapili ambapo ataweza kwenda kwa mda mrefu bila kusimama kubadili tairi hizo il hali wenzake watasimama.

Madereva wote wawili wa timu ya magari ya Redbull wamefuzu kwa kufuatana nafasi ya nne na sita.

Hata hivyo katika mbio ya kwanza wiki iliyopita huko Australia Vettel aliweza kumruka Hamilton akimaliza katika nafasi ya pili nyuma ya mshindi Jenson Button.

Timu ya magari ya Ferrari imekiri kua gari lao haliwezi kushindana na magari mengine baada ya matokeo mabovu katika mbio hizi za Malaysia na wiki iliyopita huko Australia.

Madereva Fernando Alonso na mwenzake Felipe Massa wataanza wa nane na kumi na mbili baada ya kuhangaika kujaribu kupata nafasi nzuri ya kuanza mashindano ya jumapili.