Mwanafunzi achukuliwa hatua

Christopher Samba Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Chama cha Urusi cha soka kinataka mwanafunzi aliyemrushia ndizi Samba achukuliwe hatua za kisheria

Shirikisho la soka la Urusi linataka hatua za kisheria kuchukuliwa dhidi ya mwanafunzi aliyehusika katika tukio la ubaguzi wa rangi tarehe 20 mwezi Machi, wakati alipomrushia ndizi mchezaji kutoka Congo, Christopher Samba.

Mkuu wa tume ya maadili ya shirikisho hilo anataka mhusika aadhibiwe, baada ya mwanafunzi huyo kutambuliwa wiki iliyopita.

Nchini Urusi, Samba huichezea soka klabu ya Anzhi Makhachkala.

"Tumewakabidhi wahusika wanaohusika na sheria matokeo ya uchunguzi wetu", alielezea Vasilev Vladimir.

"Ninaamini aliyefanya kosa hilo lazima aadhibiwe kwa kitendo hicho."

Samba, ambaye zamani alikuwa akiichezea Blackburn Rovers nchini Uingereza, alikuwa anaelekea katika chumba cha kubadilishia mavazi baada ya kipenga cha mwisho katika uwanja wa Lokomotiv Moscow, mechi ambayo timu yake ya Anzhi ilishindwa bao 1-0, wakati ndizi iliporushwa kutoka kwa mashabiki, na kuanguka hatua chache alipokuwa mchezaji huyo.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27, aliichukua ndizi hiyo na kuwarushia mashabiki hao, na baadaye kusema alitumaini hatua hiyo inaonyesha "haifai kuwa na tabia kama hiyo".

Mchezaji wa miaka mingi Roberto Carlos amewahi kushambuliwa kwa ndizi mara kadhaa alipokuwa akiichezea timu ya Anzi katika uwanja wa Saint Petersburg na Samara mwaka jana, jambo ambalo limewafanya wakuu wa ligi wakitaka mashabiki wasivuruge sifa za mchezo wa soka nchini Urusi.

Mchezaji wa timu ya taifa ya Nigeria na ambaye pia huichezea Spartak Moscow, Emmanuel Emenike, pia hivi majuzi alirushiwa matamshi makali ya ubaguzi wa rangi, na alitozwa faini kwa kujibu matusi hayo ya mashabiki.