Bubba Watson bingwa wa Masters

Mmarekani Bubba Watson, bingwa wa mashindano ya golf ya Masters, amesema kamwe haikumjia ndoto kwamba siku moja ataibuka mshindi wa mashindano hayo ya Augusta, nchini Marekani.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Bingwa mpya wa mashindano ya golf ya Masters ya Augusta Marekani

Watson alipambana vikali katika raundi ya mwisho dhidi ya Louis Oosthuizen, kutoka Afrika Kusini.

Watson, mwenye umri wa miaka 33, na aliyezaliwa Bagdad, jimbo la Florida mwaka 1978, alimshinda mpinzani wake mkali kutoka Afrika Kusini katika kupata pointi zaidi katika shimo la ziada, na kupata ushindi wake mkubwa wa kwanza.

"Sijawahi kupata ndoto ambayo ilifikia hatua hii, kwa hiyo siwezi kusema hii ni ndoto ambayo imetimia", alielezea mchezaji huyo, ambaye kwa kawaida hutumia mkono wa kushoto, na ambaye rasmi maishani hajawahi kupata somo lolote katika mchezo wa golf.

"Kama mchezaji golf, hii ni Mecca", alielezea.

Watson, ambaye amekuwa mchezaji wa nane kupata ushindi katika mashindano makubwa ya golf ya 'major' kwa mara ya kwanza, aliongezea: "Hili ndilo ambalo sisi hujitahidi kutimiza, kuvaa jaketi ya rangi ya kijani kibichi, kushinda mashindano yote makuu ya golf".