Man City yazinduka yailaza Norwich 6-1

Mabao matatu aliyofunga Carlos Tevez yameisaidia Manchester City kuilaza Norwich na kupunguza kasi ya pointi ya mahasimu wao Manchester United kwa pointi mbili kileleni mwa msimu wa Ligi Kuu ya England.

Haki miliki ya picha 1
Image caption Carlos Tevez alifunga mabao matatu dhidi ya Norwich

Jitahada za Tevez zilifanikiwa kumfunga mlinda mlango wa Norwich John Ruddy kabla ya kumtengenezea nafasi Sergio Aguero.

Norwich walijibu wakati Andrew Surman aliachia mkwaju ambao baadae uliokolewa na Joe Hart.

Lakini Tevez baadae akapachika bao kwa kichwa na Aguero jitahada zake binafsi akaongeza bao jingine kabla Tevez hajampiga chenga Ruddy na akakamilisha mabao yake matatu. Adam Johnson naye alibahatika kupachika bao kwa mkwaju wa karibu.

Kwa meneja wa Man City Roberto Mancini aliyedai kikosi chake hakina nafasi tena ya kunyakua tena ubingwa msimu huu na kuwapiku Man United, watakaocheza na Aston Villa siku ya Jumapuili, wachezaji wa Manchester City walionesha hawakati tamaa.

Matumaini ya kuepuka Blackburn kushuka daraja yaliangukia pua baada ya kulazwa mabao 3-0 dhidi ya Swansea.

Gylfi Sigurdsson alikuwa wa kwanza kufungua mlango wa Blackburn alipounganisha pasi ya pembeni kwa mkwaju wa mguuu wa kushoto.

Scott Sinclair alituimia makosa ya Scott Dann kumpatia pasi maridadi Danny Graham ambaye naye akamsogezea Nathan Dyer aliyepachika bao la pili.

David Dunn alikosa nafasi nzuri ya kuipatia Rovers bao la kufutia machozi, kabla ya Dann kujifunga mwenyewe baada ya Sigurdsson mkwaju wake kugonga mwamba.

Hali si nzuri kwa Blackburn chini ya meneja Steve Kean ambaye kikosi chake kinaonekana dhahiri kuteremka daraja msimu huu wakiwa pointi tatu nyuma ye eneo la hatari.

Mchezo wa ovyo uliooneshwa na Queens Park Rangers wakicheza ugenini uliwasababishia kupoteza mchezo kwa kufungwa bao 1-0 na sasa wapo pointi mbili tu kuelekea eneo la kuteremka daraja.

Bao la Graham Dorrans alilofunga kipindi cha kwanza liliifanya QPR kuweka kibindoni pointi mbili tu katika mechi 11 ilizocheza ugenini.

Billy Jones mkwaju wake uligonga nguzo kipindi cha pili lakini QPR watajutia nafasi ambazo walizipoteza katika pambano hilo.

Bobby Zamora alipoteza nafasi tatu ambapo mara mbili mikwaju yake iliokolewa na mlinda mlango Ben Foster, na pia alikaribia kufunga kwa kichwa.

Wolves ilizuia wimbi la kupoteza mchezo wa saba mfululizo baada ya kulazimisha sare ya kutofungana na Sunderland katika uwanja wa Stadium of Light, lakini hata hivyo wameendelea kushikilia mkia wa Ligi Kuu ya England.

Sunderland walikuwa na nafasi nzuri kufunga kipindi cha kwanza, James McClean alifyatua mkwaju uliogonga nyavu za pembeni mwa lango baada ya kuambaa na mpira vizuri.

Lakini Sunderland baada ya kipindi cha pili hawakuonesha juhudi zaidi kutafuta mabao na Wolves walionekana kama wangeshinda pambano hilo ambapo mpira wa kichwa uliopigwa na Steven Fletcher uliokolewa na mlinda mlango Simon Mignolet.

Ni namna gani meneja wa Wolvea Terry Connor atamaliza kadhia hii ya kuendelea kusalia mkiani ni mwenyewe anavyojua.

Alipoteuliwa mwezi wa Februari zikiwa zimesalia mechi 13, Wolves ilikuwa ni moja ya vilabu vitatu vilizokuwa na pointi 21 pamoja na Bolton na Wigan.