Liverpool 2 Everton 1

Luis Suarez Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Suarez aliifungia Liverpool bao la kwanza katika nusu fainali

Bao la Andy Caroll katika dakika za mwishomwisho za mechi ya nusu fainali ya Kombe la FA dhidi ya Everton katika uwanja wa Wembley, limeiwezesha Liverpool kuingia fainali ya Kombe la FA.

Nikica Jelavic alitumia nafasi nzuri iliyojitokeza wakati wachezaji wa Liverpool Jamie Carragher na Daniel Agger walipokosa mawasiliano na kujichanganya, na kuiwezesha Everton kupata bao la kwanza katika mechi hiyo.

Sylvain Distin naye hakuisaidia Everton wakati alipompigia kipa wake Tim Howard mpira wa kurudisha nyuma, kwani Luis Suarez aliitumia nafasi hiyo kuutumbukiza mpira wavuni.

Na huku zikisalia dakika tatu mpira kumalizika, Carroll, ambaye awali alikuwa amekosa nafasi nzuri za kufunga mabao katika kipindi cha pili, aliweza kuuelekeza mpira wavuni kwa kichwa.

Liverpool sasa imejiweka katika nafasi nzuri ya kuweka mkobani Kombe la FA, baada ya tayari kuweka kibindoni Kombe la Carling.