Fabrice Muamba aondoka Hospitalini

Haki miliki ya picha 1
Image caption Fabrice Muamba na maafisa wa Bolton

Mwanasoka wa Uingereza ,Fabrice Muamba, ambaye nusura afe baada ya moyo wake kusimama ameruhusiwa kwenda nyumbani.

Muamba amekuwa akipokea matibabu katika hospitali ya moyo mjini London. Kiungo huyo wa Bolton Wanderers alianguka uwanjani wakati klabu hiyo ikicheza na Tottenham kufuzu kwa nusu fainali za kombe la FA.

Amekuwa akisaidiwa na daktari aliyempa huduma ya kwanza alipoanguka uwanjani. Muamba amewaambia waandishi wa habari kwamba anatarajia kupata muda na familia yake huku akiwarudishia shukurani mashabiki na wenzake ambao waliungana naye wakati wote akiwa hospitalini.

Hapo Jumamosi shirikisho la soka Italia lilisimamisha mechi zote baada ya mchezaji wa klabu ya Livorno, Piermario Morosini, kuzirahi na baadaye kufariki dunia alipokuwa akichezea klabu yake.