Jack Wilshere kukosa fainali Euro 2011

Kiungo wa Arsenal na timu ya taifa ya England Jack Wilshere, hataweza kusakata kabumbu hadi msimu huu utakapomalizika na hatakuwa katika hali nzuri kuiwakilisha England katika fainali za Euro 2012.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Jack Wilshere kukosa michuano ya Ero 2012

Wilshere mwenye umri wa miaka 20 alivunjika kifundo cha mguu wakati wa mechi za kujipasha moto kabla ya kuanza msimu huu na alikuwa na matumaini ya kupona haraka ili aiwakilishe timu yake ya taifa kule Poland na Ukraine.

Wilshere aliandika kupitia mtandao wa jamii wa tweeter siku ya Jumatatu: "Nimesikitishwa, mbaya sana na nimehuzunika.

"Lilikuwa ni jaribio la kiakili kwangu msimu huu na hali itaendelea kuwa ngumu hadi nitakaporejea uwanjani."

Amewashuru mashabiki kwa kumuunga mkono na akaongeza: "Kifundo changu cha mguu kipo sawa, bado nina matatizo tu madogo-madogo na kwa vile nimekuwa nje kwa muda mrefu sitakuwa tayari kucheza fainali za Euro.

"Nina matumaini England itaweza kufanya vizuri na kuleta kombe nyumbani! Nitaangalia na kuwashangilia wenzangu nikiwa mshabiki halisi wa England!"

Akimzungumzia Wilshere baada ya Arsenal kuangukia pua walipochapwa na Wigan uwanja wao wa Emirates, meneja Arsene Wenger alisema: "Hayupo tayari kufanya mazoezi leo au wiki ijayo. Anaendelea vizuri, lakini polepole.

"Hatakuwa tayari hadi mwishoni mwa msimu huu na pia kwa fainali za Euro. Amevunjika moyo na unaweza kuelewa hilo.

Wilshere hajaichezea Arsenal tangu alipoumia katika mechi ya kirafiki dhidi ya New York Red Bulls tarehe 31 mwezi wa Julai mwaka jana.

Mashindano ya kutafuta bingwa wa Ulaya yataanza Poland tarehe 8 mwezi wa Juni na England itaanza heka heka za kulinyakua kombe hilo tarehe 11 mwezi huo wa Juni itakapooneshana kazi na Ufaransa.

Kulikuwa na dalili Wilshere angeweza kuichezea Arsenal katika michezo mitatu ya kumaliza msimu wa ligi dhidi ya Stoke, Norwich na West Brom ikiwa ni maandalizi yake kutafuta nafasi katika kikosi cha England kwa ajili ya fainali za Euro 2012.

Lakini Wenger kila mara alikuwa akiweka wazi asingemruhusu kuichezea England iwapo kwa kufanya hivyo ingekuwa hatari kwake kujitonesha.

Wenger pia amefuta matumaini ya Wilshere kuwemo katika kikosi cha Uingereza kitakachocheza mechi za kandanda za Olimpiki, zitakazoanza tarehe 26 mwezi wa Julai ambazo zitaingiliana na mechi za ufunguzi wa msimu mpya wa Ligi.