Mafundi wa Force India watoroka

Timu ya Force India Haki miliki ya picha AP
Image caption Madereva wanahofia ghasia katika mashindano ya magari ya Sakhir Bahrain

Timu ya mashindano ya langalanga ya Force India ilibidi kukwepa mabomu ya petroli iliyorushiwa, wakati ilipokuwa ikirudi katika kituo chake, baada ya kufanya mazoezi katika mashindano ya Bahrain.

Mafundi wanne waliokuwa katika gari hilo ilibidi kujaribu kukwepa ghasia, baada ya polisi kuanza kushambuliana na waandamanaji.

Gesi ya kutoa machozi iliyorushwa na polisi ilipenya na kuingia gari lao, lakini walifanikiwa kutoroka kwa kupata fursa katikati ya ndimi za moto barabarani.

Hakuna mtu katika timu ya Force India aliyejeruhiwa, lakini kuna watu wawili wa timu hiyo wameomba kurudi nyumbani.

Baadhi ya timu zilitazamia kwamba mashindano ya mwaka huu yatafutiliwa mbali, lakini chama cha mchezo huo duniani, FIA, kimesisitiza kwamba mashindano yataendelea.

Mazoezi ya kwanza katika kujiandaa kwa mashindano ya Jumapili yatafanyika Ijumaa, saa moja asubuhi, kwa saa za GMT.

Timu hiyo ya Force India ilishambuliwa katika barabara kuu ilipokuwa ikirudi katika mji mkuu wa Manama.

Maandamano ya makundi yaliyokuwa yakiipinga serikali yalisababisha mashindano ya mwaka 2011 nchini humo kutofanyika, na baadhi ya timu mwaka huu zimetazamia hatua kama hizo kuchukuliwa, kwa kuhofia usalama wao.

Lakini licha ya wasiwasi wao, hakuna timu ambayo imejitokeza waziwazi kupinga uamuzi wa chama cha mchezo huo kuamua kwamba mashindano ya Bahrain bado yatafanyika.