Torres afunga matatu, Blackburn hatarini

Fernando Torres amepachika mabao matatu murua na kuweka hai matumaini ya Chelsea kumaliza katika nafasi nne za juu za msimamo wa Ligi Kuu ya Kandanda ya England, walipoilaza QPR mabao 6-1 ambao wapo hatarini kushuka daraja.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Fernando Torres akishangilia moja ya mabao yake akiwa na John Terry

Daniel Sturridge alikuwa wa kwanza kufungua karamu ya mabao mapema tu sekunde ya 45 na baadae John Terry akapachika bao la pili kwa kichwa akifuatiwa na Torres aliyeweka wavuni mabao mawili ya haraka haraka na kuifanya Chelsea kuwa mbele kwa mabao 4-0 hadi dakika 25 kipindi cha kwanza.

Torres alikamilisha mabao yake matatu baada ya mapumziko na Florent Malouda akafunga kitabu kwa kuandika bao la sita kabla ya Djibril Cisse kuipatia QPR bao moja la kufutia machozi.

Matokeo hayo yameibakisha Chelsea katika nafasi ya sita huku QPR ikiwa juu ya mstari wa kuteremka daraja kwa tofauti ya mabao na Bolton.

Katika mchezo mwengine Tottenham imefanikiwa kujiinua hadi nafasi ya nne ya msimamo wa Ligi Kuu ya Kandanda ya England baada ya kuilaza Blackburn mabao 2-0. Blackburn wana wasiwasi mkubwa wa kuteremka daraja msimu huu na kufungwa kwao kumewazidishia hofu hiyo.

Rafael van der Vaart alitangulia kuipatia Spurs bao la kwanza kwa kwaju wa karibu baada ya mpira wa kichwa uliopigwa na Gareth Bale kugonga mwamba wa lango la Blackburn.

Kyle Walker akiwa umbali wa yadi 25 aliachia mkwaju wa adhabu ya moja kwa moja na mpira ukaenda moja kwa moja wavuni na kuipatia Spurs bao la pili dhidi ya Rovers ambao wapo nafasi ya pili kutoka mkiani na hawakuonesha mchezo wowote wenye nia ya ushindi.