Gicharu afuzu Morocco

Benson Gicharu na John Nene
Image caption Bondia Benson Gicharu kutoka Kenya ni kati ya mabondia waliofuzu nchini Morocco

Mabondia watatu wa Kenya, Benson Gicharu, Daniel Shisia na Charles Okoth, wanabeba matumaini ya mabondia wa Afrika Mashariki na Kati kwenye mashindano ya ndondi kwa mataifa ya Afrika ya kufuzu kwa michezo ya Olympiki ambayo yanaingia hatua ya nusu-fainali Ijumaa wiki hii mjini Casablanca, Morocco.

Gicharu, mshindi wa medali ya fedha michezo ya Jumuiya ya Madola, anapambana na Duke Micah wa Ghana uzani wa fly, Shisia anaingia ulingoni kuzipiga na Maxwell Amponsah wa Ghana uzani wa heavy naye Okoth, ambaye anasomea uanasheria mjini Nairobi, anazipanga na Mohammed Arjaoui wa Morocco uzani wa super-heavy.

Hao ndio mabondia wa mataifa ya Afrika Mashariki na Kati waliobaki mashindanoni.

Wawili wa Tanzania Emiliani Polino uzani wa bantam na Selemani Kidunda uzani wa welterweight waling'olewa Jumatano wiki hii huku kocha mkuu wa timu ya Tanzania Michael Changarawe akidai bondia wake alishinda lakini waamuzi wakaegemea upande wa mpinzani wake Mehdi Khalsi wa Morocco.

''Hapa kuna njama ya kusaidia mabondia wa mataifa ya Afrika Kaskazini kufuzu kwa michezo ya Olympiki.

Itakuwaje bondia wa Morocco anapata pointi zote hizo na amerusha makonde machache sana,'' alisema Changarawe ambaye pia ni kaimu mwenyekiti wa chama cha ndondi cha Tanzania.

Kocha wa Nigeria Prince Idika Nsofor naye pia amelalamika kuhusu waamuzi, akisema bondia wake Hima Moustapha alinyolewa bila maji aliposhindwa na IIlaya Abadi wa Algeria hatua ya robo-fainali.

Amependekeza mataifa ya Afrika ya kutoka magharibi, mashariki na kusini kwa miaka ijayo yawe na mashindano yao ya kufuzu kwa michezo ya Olympiki kutokana na kile anachokitaja kama njama ya kusaidia mataifa ya Afrika Kaskazini kupeleka mabondia wengi zaidi London.

Baadhi ya mabondia chipukizi ambao wametia fora zaidi kufikia sasa ni Isaac Dogboe wa Ghana, mwenye umri wa miaka 17 anayekutana na Siyabonga Sonjica wa Afrika Kusini uzani wa bantam kwenye nusu-fainali.

Dogboe ni mwanafunzi mjini London.