Rangers kumilikiwa na Mmarekani

Rangers
Image caption Klabu ya Rangers iliyozongwa na madeni sasa kumilikiwa na tajir wa Marekani Bill Miller

Wanaosimamiwa klabu ya Rangers, wamekubali tajiri wa Marekani, Bill Miller, kuendelea na mipango ya kuinunua klabu, na wanatumaini kufikia mwisho wa msimu atakuwa ni mmiliki mpya.

Mfanyibiashara huyo wa Marekani ana mipango ya kuanzisha kampuni mpya, na akiwa na nia ya kuzihamisha rasilmali za Rangers hadi kampuni hiyo mpya.

Gharama za kuinunua Rangers zilitegemea masharti ya kiuchumi ambayo klabu hiyo ingelitozwa na chama cha soka cha Uskochi.

Lakini sasa kampuni inayosimamia uuzaji huo, Duff & Phelps, imeelezea kwamba hamna masharti zaidi sasa.

"Bill Miller sasa ameridhika na masharti ya chama cha soka na hamna tena vikwazo na ombi lake, na kwa hali hiyo, tunaweza kuendelea", alielezea David Whitehouse, ambaye ni msimamizi wa pili anayeshirikiana na kuisimamia klabu ya Rangers.

Shughuli ya kuiuza klabu ilianza tarehe 14 Februari mwaka huu.

Rangers waliadhibiwa kwa kupunguziwa pointi 10 kutoka ligi kuu ya Premier ya Uskochi, na wasimamizi wakaamua mishahara kupunguzwa.

Klabu kilikosa kutimiza masharti ya shirikisho la soka barani Ulaya la UEFA kupata leseni ya kushiriki katika mashindano msimu huu, lakini tayari wamewasilisha ombi la kushirikishwa katika mechi za Ulaya msimu ujao.

Mahasimu wao wakubwa Celtic tayari walitangazwa kuwa mabingwa wa ligi kuu ya Uskochi msimu huu, tarehe 7 mwezi Aprili, huku wakiwa katika nafasi ya pili, na wakiwatangulia Motherwell kwa zaidi ya pointi 8, na bado wana mechi mbili.

"Bw Miller sasa anatumaini kumaliza shughuli nzima kufikia mwisho wa msimu", alielezea Whitehouse.

Chama cha soka cha Uskochi na pia wasimamizi wa ligi kuu ya Premier ya Uskochi wanapanga kufanya mashauri zaidi na Miller, ambaye utajiri wake ulitokana na biashara ya kuvuta magari yaliyokwama.