Capello atamani ligi ya England

Haki miliki ya picha Getty
Image caption FabioCapello anataka kufundisha timu ligi kuu ya England

Kocha mkuu wa zamani wa timu ya taifa ya England Fabio Capello sasa anataka kufundisha moja ya vilabu vya England vinavyoshiriki ligi kuu ya nchi hiyo.

Kocha huyu mwenye miaka 65 alijiuzulu kuwa Kocha mkuu wa England mwezi Februari mwaka huu na sasa anaonekana kutaka kupata uongozi katika moja ya vilabu vya nchi hiyo.

"Najua England itakuwa furaa nzuri kwangu maana nazifahamu vyema timu pamoja na wachezaji wa nchi hiyo". Capello aliliambia gazeti la Times.

''Ningependa kuongoza timu ambayo inataka kushinda taji fulani, kama inawezekana.''

Tayari Capello ameshakataa kufunza timu zingine za nje ya England, huku meneja huyo wa zamani wa AC Milan akijiandaa kwa nafasi ya kufundisha moja ya vilabu vikubwa England.

Kocha huyo raia wa Italia anaonekana kuziba mianya ya kufundisha vilabu vingine baada ya sasa kuonekana kujielekeza moja kwa moja kutaka kufundisha vilabu vyenye nafasi ya kucheza ligi kuu ya mabingwa Ulaya na inaweza kunyakua ubingwa wa ligi kuu ya England.

"Ningefurahia zaidi ubora wa timu na sio pesa. Sifanyi kazi kwa ajili ya fedha," aliongeza.

Wakati huo huo Capello anaonekana kuunga mkono uamuzi wa Chama cha Soka cha England FA cha kumteua Roy Hodgson kuwa mrithi wake.